BoT yakemea wenye tabia za kuunganisha noti kwa pini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wote wenye tabia ya kuunganisha noti pamoja kwa kutumia pini au stempu pini kuacha mara moja, kwani kufanya hivyo kutasababisha uharibifu wa fedha na kuchakaa haraka.
Hayo yamesemwa leo Februari 26,2025 na Afisa wa Benki Kuu kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu, Bi. Itika Mwakisambwe wakati akiwasilisha mada ya historia ya fedha za Tanzania, alama za usalama na utunzaji wa fedha hizo katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na masoko ya fedha.

Semina hiyo ya siku tatu ambayo imeratibiwa na BoT kuanzia Februari 25, 2025 hadi Februari 27,2025 inaendelea katika tawi la BoT mkoani Mtwara.

Pia, amesema kila mmoja anapaswa kuacha au kupunguza kuzikunja fedha za noti. "Kwani, kukunja kupita kiasi kunadhoofisha karatasi na inaweza kukatika.

"Na fedha, zishikwe tukiwa na mikono safi na mikavu, tutambue asilimia 100 ya noti zetu zinatengenezwa kwa pamba, hivyo ukizishika na mikono michafu zinachafuka na kuharibika.

"Kwa hiyo, tunapaswa kuithamini, na kuitunza vizuri fedha yetu ili ziweze kudumu katika mzunguko."
Katika hatua nyingine, Afisa huyo wa BoT amesema kuwa,kuzikukunja noti na kuziandika au kuchana pembeni hakukubaliki, kwani huo ni uharibifu wa fedha na inaporudi Benki Kuu inaharibiwa, hivyo kusababisha hasara kwa Serikali.

Ikumbukwe, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitumia gharama kubwa ya fedha za kigeni kutengeneza fedha zinazotumika hapa nchini.

Kutokana na sababu hiyo, Benki Kuu ina wajibu wa kuhakikisha kuna fedha safi katika mzunguko muda wote, hivyo uharibifu wowote ule wa fedha hauvumiliki na haukubaliki nchini.

Aidha, utunzaji mzuri wa shilingi ya Tanzania uwezesha kukaa katika mzunguko wa shughuli za kiuchumi kwa muda mrefu, hivyo gharama ambazo zingetumika kutengeneza fedha mpya kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu, maji, afya, elimu na mingineyo.

Pia, amewataka wananchi kutozitunza noti au sarafu ndani badala yake waziingize katika mzunguko au kuziweka katika taasisi za fedha ili ziendelee kuwa katika uzalishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news