BoT yatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za Programu Tumizi (Apps) zinazotoa mikopo kinyume na taratibu

MTWARA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za programu zinazotoa mikopo kidijitali pamoja na huduma za kifedha kinyume na taratibu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Wito huo umetolewa na Afisa Mkuu Mwandamizi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Bw. Deogratias Mnyamani, wakati akiwasilisha mada katika semina kwa waandishi wa habari inayoendeshwa na Benki Kuu katika tawi lake mkoani Mtwara.

Bw. Mnyamani amesema Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka zingine wamefanikiwa kuzifungia taasisi zaidi ya 70 ambazo zilikuwa zikitoa mikopo kinyume na taratibu, na wataendelea kuzifungia taasisi hizo kadri zitakavyogundulika.

“Taarifa mnazotakiwa kuripoti ni pamoja na jina la mtoa huduma au mhusika wa programu inayotumika kukopesha, mahali wanapopatikana pamoja na mawasiliano ya mkopeshaji,” amesema.

Aliongeza kuwa Benki Kuu inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za fedha na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wakopeshaji halali pamoja na uwazi katika riba na tozo zingine.

Mwananchi anapaswa kuzingatia mambo muhimu kabla ya kuchukua mkopo ili kuepuka changamoto za kifedha. Kwanza, ni muhimu kuhakikisha anakopa kutoka kwenye taasisi yenye leseni ya Benki Kuu ili kuepuka taasisi zisizo rasmi ambazo zinaweza kuwa na masharti yasiyo rafiki.

Pia, anatakiwa kusoma, kuelewa, na kuzingatia vigezo na masharti ya mkataba wa mkopo kabla ya kusaini, pamoja na kuchukua nakala ya mkataba kwa ajili ya kumbukumbu.

Aidha, ni jukumu la mkopaji kurejesha mkopo kwa wakati ili kuepuka gharama za ziada au athari mbaya za kifedha. Mkopo unapaswa kuchukuliwa kwa malengo maalum na kutumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Endapo mkopaji atakutana na changamoto au ana malalamiko kuhusiana na huduma za kifedha, anashauriwa kuwasiliana na Dawati la Malalamiko ya Wateja wa Huduma za Kifedha lililopo Benki Kuu.

Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kupitia barua pepe ya Benki Kuu, mitandao ya kijamii, au kwa kutembelea ofisi za Benki Kuu zilizo karibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news