DODOMA-Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umewaonya wanafunzi na watu wengine wanaojaribu kudukua mifumo ya chuo hicho na kwamba yeyote atakayethubutu kufanya hivyo chuo kitambaini kutokana na kuwa na wataalamu wabobevu wa Tehama na atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Rose Joseph ameeleza hayo leo chuoni hapo wakati akizungumzia sakata la wanafunzi 121 waliofutwa chuoni hapo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika kuchezea mfumo wa matokeo ya mitihani (SR2).
“Tumeweza kubaini kwenye mojawapo ya ‘social media’ hizi WhatsApp kwamba wanafunzi wanatumiwa vitaarifa kwamba kuna mtu ana uwezo wa kubadilisha taarifa zao kwenye mifumo, kwa hiyo unakuta wengi kwa sababu ya uvivu wa kusoma au kwa sababu ya kutokuona kwamba hawawezi kufanya vizuri, wakaingia kwenye mtego wa namna hii bila kubaini kwamba chuo kina misingi na mifumo mizuri zaidi, na kwa sababu tunafanya vizuri zaidi kwenye Tehama lazima watambue kwamba tuna wataalamu wabobevu, kwa hiyo vitendo kama hivi vya kudukua mifumo lazima tutawabaini.”
Jumla ya wanafunzi 121 wa chuo hicho wamefutwa masomoni baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika kuchezea mfumo wa matokeo ya mitihani (SR2).
Wanafunzi hao walituhumiwa kuchezea mfumo huo mwaka 2023/2024 ambapo Serikali iliunda kikosi kazi kilichohusisha wataalamu wa mifumo ya kompyuta kuchunguza tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yao Chuo Kikuu cha Dodoma.
Aidha, baada ya chuo kupokea ripoti hiyo hatua za ndani zilianza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapa wito watuhumiwa kwenda kusikilizwa kabla ya kutoa maamuzi kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Awali taarifa iliyotolewa na chuo hicho imeeleza kuwa jumla ya wanafunzi 170 walituhumiwa kuchezea mfumo huo ambapo kati ya hao wanafunzi 138 walisikilizwa, wanafunzi 32 hawakufika kusikilizwa.
Katika wanafunzi waliosikilizwa, wanafunzi 121 walipatikana na hatia ya kuhusika kuchezea matokeo ya mitihani na kikao cha Seneti ya Chuo kupitisha kuondolewa masomoni (Discontinue) na kwamba kesi za wanafunzi 15 zinaendelea na uchunguzi zaidi ambapo wanafunzi wawili hawakukutwa na hatia na wanaendelea na masomo.