KILIMANJARO-Wataalamu wa Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zake wametakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu mbinu bora za kusimamia fedha zao ili kuepuka kuingia kwenye mikopo yenye masharti magumu.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mhe. Raymond Mwangwala, alitoa wito huo alipokutana na Timu ya Wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi zake, walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kuanza kampeni ya utoaji elimu kwa wakazi wa Wilaya hiyo.
Mhe. Mwangwala alieleza kuwa mikopo yenye riba kubwa imekuwa mzigo kwa wananchi, hasa wanawake, na kusababisha matatizo ya kifamilia kwa kuwa baadhi yao wanakopa bila kuwashirikisha wenza wao na alihimiza elimu hiyo kutolewa kwa watumishi wa halmashauri ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kabla ya kustaafu, na kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa suala hili na kupeleka wataalamu wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), UTT AMIS na NSSF kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alieleza kuwa elimu hiyo inalenga kuwafikia watumishi, wananchi na wanafunzi ili waweze kujifunza njia bora za kuhifadhi fedha zao, kupata faida, na kukopa kwa njia salama kwa kufuata taratibu rasmi.

Naye Mratibu wa Huduma za Fedha wa Wilaya ya Rombo, Bi. Monica Kilawe, alikiri kuwepo kwa changamoto ya taasisi binafsi zinazotoa mikopo bila kufuata taratibu, hali inayosababisha madhara kwa wananchi.
Timu hiyo ya wataalamu imetembelea tarafa zote na kata 28 za Wilaya ya Rombo, ikitoa mwongozo wa jinsi ya kuepuka mikopo hatarishi na kuweka misingi thabiti ya usimamizi wa fedha.