DAR-Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na SoftVentures, Tume ya TEHAMA (ICTC) na Chama cha Watoa Huduma za Intaneti Tanzania (TISPA), inatangaza kuingia ushirikiano wa kimkakati na Deloitte kwa ajili ya Tuzo za TEHAMA 2025, pamoja na matokeo ya uteuzi wa kazi za washiriki wa tuzo hizo ambayo hayajawahi kushuhudiwa.
Deloitte inajiunga na Tuzo za TEHAMA ili kuimarisha utawala na uaminifu wa tuzo hizi.

Miongoni mwa mambo ambayo yatafanywa na kampuni hiyo ni kutoa ushauri na usimamizi katika mchakato wa tathmini.
Pia,kusaidia katika usimamizi wa utawala na hatari na kuchangia maarifa ya sekta ili kuendeleza mabadiliko ya kidijitali Tanzania.
"Deloitte inajivunia kushirikiana na Tuzo za TEHAMA 2025 katika kutambua na kusherehekea ubora wa TEHAMA nchini Tanzania.
"Ushirikiano huu unaonesha dhamira yetu ya kukuza uvumbuzi, utawala bora,na ukuaji endelevu wa kidijitali,"amesema Suzana Patrick, Mshauri Mwandamizi wa Deloitte.
Akizungumzia ushirikiano huu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema; "Kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya Tuzo za TEHAMA, tunaamini kuwa utawala imara na uwazi ni muhimu katika kutambua ubora halisi katika sekta ya TEHAMA.
"Ushirikiano na Deloitte kwa Tuzo za TEHAMA 2025 unathibitisha dhamira yetu ya kuhakikisha viwango vya juu zaidi katika mchakato wa tathmini.
"Ushirikiano huu unahakikisha kuwa uvumbuzi, athari, na uadilifu vinabaki kuwa msingi wa tuzo hizi tunaposherehekea wale wanaobadilisha mustakabali wa kidijitali wa Tanzania."
Idadi Kubwa ya Uteuzi
Wakati huo huo,tuzo hizo zimepokea uteuzi wa kazi 380 katika vipengele 10, huku kukiwa na ushiriki mkubwa katika vipengele vidogo 21 kati ya 22. Maeneo makuu ya ushindani ni pamoja na:
■Matumizi ya TEHAMA katika Elimu, Fedha, na Afya
■Uvumbuzi wa Usalama wa Mtandao
■Mbinu Bora za Ulinzi wa Taarifa
■Teknolojia Zinazochipukia
■Miradi ya TEHAMA katika Sekta ya Umma na Binafsi
■Tuzo za Muunganisho wa Mtandao (Mtoa Huduma Bora wa Mawasiliano, ISP, na MNO)
■Utofauti katika Teknolojia (Mvumbuzi Mwanamke, Kiongozi wa Teknolojia Mwanamke,Ubora wa Wanafunzi)
Hafla ya utoaji tuzo kusherehekea mafanikio ya TEHAMA nchini Tanzania inatarajiwa kufanyika Februari 21,2025 katika Ukumbi wa Hotel Gran Meliá, Arusha.
Hatua inayofuata ni ukaguzi na uchunguzi wa uteuzi na tathmini ya jopo la majaji, huku orodha ya shiriki watakaingia hatua ya fainali ikitarajiwa kutangazwa hivi karibuni.