Dkt.Mpango afanya mazungumzo na watendaji wakuu wa Innovo na MECCO

DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Innovo ya nchini Uingereza, Bw. Paul Woodman pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya MECCO Bw. Nasser Sheikh, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Februari 17, 2025.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameikaribisha kampuni ya Innovo kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu kama vile barabara na reli pamoja na miundombinu ya nishati ya umeme ikiwemo umeme wa jua, upepo na jotoardhi. Pia amesema fursa ipo katika kuwekeza miundombinu ya afya kama vile ujenzi wa hospitali pamoja na usimamizi wa taka.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ni nchi bora zaidi katika uwekezaji kwa kuwa uchumi wake ni himilivu na unakuwa kwa kasi kusini mwa Jangwa la Sahara. Ameongeza kwamba eneo la kijiographia la Tanzania ni fursa katika kuhudumia mataifa mengine ambayo hayana bahari hivyo kuchagiza biashara na maendeleo.

Kampuni ya Innovo ya Uingereza imekuwa ikifadhili na kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Bara la Afrika kama vile ujenzi wa barabara, hospitali na viwanja vya ndege.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Ujenzi wa Ujenzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia katia ya Serikali na Sekta Binafsi,David Kafulila pamoja na Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi John Ulanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news