DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Februari 19,2025.

Ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya Elimu, Miundombinu, TEHAMA, Afya, Kilimo, Viwanda na Nishati.
Amesema makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Korea katika madini ya kimkakati yataleta manufaa mengi zaidi kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini mengi ambayo yanaenda sambamba na mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo inajikita katika uchumi wa teknolojia za kijani.
Aidha,Makamu wa Rais amemueleza Balozi wa Jamhuri ya Korea umuhimu wa kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Korea yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Amesema, uongezaji wa thamani kwa malighafi hapa hapa nchini utachochea biashara, uhamishaji teknolojia pamoja ongezeko la ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Pia,Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Jamhuri ya Korea katika kubadilishana wafanyakazi, ambapo amemsihi Balozi huyo kuwezesha mchakato wa kujiunga katika Mfumo wa Vibali vya Ajira (EPS) ili wafanyakazi wa Tanzania waweze kuingia katika soko la ajira la Korea na kufanya kazi katika sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa meli, sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa.
Halikadhalika amesema ushirikiano unahitajika katika Elimu na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya kwa kuwapatia mafunzo katika ubingwa na ubobezi wa utoaji matibabu mbalimbali. Makamu wa Rais pia amesisitiza kushirikiana katika masuala ya utamaduni, michezo na lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn amesema katika kipindi atakachohudumu nafasi ya Ubalozi nchini Tanzania, atahakikisha anasimamia na kuharakisha kukamilika kwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ikiwemo ushirikiano katika madini ya kimkakati na maendeleo ya uchumi wa buluu.