Dkt.Yonazi awakumbusha watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutekeleza majukumu kwa weledi

DODOMA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amewakumbusha watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ushirikiano, upendo, furaha na amani ili kuyafikia malengo ya ofisi hiyo.
Dkt. Yonazi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi Ofisi yake wakati wa mkutano wake na watumishi hao uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo Njedengwa jijini Dodoma leo Februari 4, 2025.

Dkt. Yonazi amesema ipo haja ya kila mtumishi kujifanyia tathmini katika utendaji wakewa kazi huku akizingatia miongozo na kanuni za utumishi wa umma na kusema kuwa, kila mtumishi anawajibika katika kuhakikisha ofisi inapata matokeo iliyoyakusudia na kwa ufanisi.
“Ni wakati sahihi kila mmoja kuilinda furaha aliyonayo awapo mahali pa kazi, isingefaa utoke nyumbani huna furaha na ufike eneo la kazi ukose furaha, ni vyema kuja eneo la kazi na kuipate furaha mara mbili kwa kuzingatia mazingira yaliyorafiki katika kutekeleza majukumu,” alisema Dkt. Yonazi.

Aliongezea kuwa kila mtumishi wa umma awe na desturi ya kuheshimu nafasi ya mwingine bila kujali tofauti zinazoweza kuwepo miongoni mwa watumishi hao.

“Ni vyema kila mtu akajali mwingine na ikumbukwe hakuna mtu mwenye uwezo mdogo wa kufanya kazi, jambo la msingi ni kuhakikisha ule uwezo uliopewa na Mwenyezi Mungu na Mafunzo mbalimbali unatumia vizuri na kuhakikisha uleta matunda mazuri na kuleta maendeleo kwa Nchi yetu,” alisema Dkt. Yonazi.
Sambamba na hilo aliwaeleza watumishi hao kuwa kila mmoja ni kiongozi katika eneo lake la kazi hivyo abebe dhamana hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa.

“.....kila mtumishi aliyepo hapa ndiye Katibu Mkuu kwenye eneo lake, kwa kubeba imani ya kwamba ni Katibu Mkuu anapaswa kuwa na nidhamu na bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kuwa mwaminifu,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. James Kilabuko katika neno lake la utangulizi amewaasa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuzingatia sheria za utumishi wa Umma huku akiwasihi kuimarisha umoja na mshikamano ili kuiletea Serikali maendeleo yake.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Waziri Mkuu Bi, Numpe Mwambenja ameomba watumishi kuendelea kujitathimini mienendo yao katika utumishi wa Umma kwa kufanya kazi vizuri na nidhamu na kuheshimu viongozi huku wakiheshimiana wao kwa wao.
Bi. Numpe alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna unavyojali maslahi ya watumishi na ustawi wao kwa ujumla na kuwasihii watumishi kuendelea kutimiza wajibu kwa kuzingatia kauli ya “hakuna haki bila wajibu”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news