DPWorld yafunguka kuhusu upotoshaji huu

TAARIFA KWA UMMA

Kumetokea taarifa zisizo sahihi kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na DPWorld kwa kampuni za meli za Emirates Shipping Line na MSC -Mediteranean Shipping Company kuwa hafifu.Tunautaarifu umma kuwa habari hizo hazina ukweli wowote.
Bandari ya Dar Es Salaam ina magati kumi na moja: gati namba 0-7 yanayoendeshwa na kampuni ya DPWORLD na yanahudumia meli za magari, meli za mzigo wa kichele, meli za mzigo mchanganyiko, na meli za makasha.

Gati namba 8 hadi 11 yanaendeshwa na mtoa huduma mwingine na yanahudumia meli za makasha pekee.

Tunatoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Kampuni ya meli ya Emirates Shipping Line haitumii huduma za kampuni ya DPWorld Dar Es Salaam. Kampuni ya MSC -Mediteranean Shipping Company inatumia huduma za DPWorld Dar Es Salaam.

Jumla ya meli za makasha zilizohudumiwa Mei 2024 hadi Januari 2025 zilikuwa 97 na makasha zaidi ya 217,000 yaliyochangia bandari ya Dar Es Salaam kuvunja rekodi kwa kuhudumia makasha zaidi ya milioni 1 kwa mwaka 2024. Hii ni ongezeko la asilimia 5 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023.

Kabla ya kampuni ya DPWorld Dar Es Salaam kuanza kazi, bandari ya Dar Es Salaam ilikuwa inapokea meli 3 hadi 4 za MSC kwa mwezi za MSC.

Kufuatia na ongezeko la ufanisi kwenye huduma inayotolewa na DPWorld ambalo limepelekea meli za makasha kuingia bandarini bila kusubiri nje zaidi ya siku mbili na wakati mwingine kuingia moja kwa moja, kampuni ya MSC ilitangaza kuondoa tozo ya ucheleweshwaji (vessel delay surcharge) mwishoni mwa mwezi Disemba ambayo imewapunguzia waagizaji takribani dola za kimarekani 500 kwa kila kasha.

Kuanzia mwezi Januari MSC inaleta meli mara nane kwa mwezi zikiiunganisha bandari ya Dar Es Salaam kwa safari za moja kwa moja kutoka India, Singapore na Afrika Kusini ambayo imepunguza muda wa mzigo kuwasili nchini na kuchochea biashara.

Meli iliyolalamikiwa mtandaoni ya MSC Imma ilikuwa na makasha 150 tu kwa ajili ya Dar Es Salaam na ilipangwa kutokuingia bandarini kwa maombi ya kampuni ya MSC.

Tunatumia fursa hii kuwashukuru wadau wa bandari ya Dar Es Salaam ambao wameendelea kuonesha ushirikiano mkubwa uliojidhihirisha kwenye ukuaji wa mzigo kwa asilimia 12.

Tunashauri wadau kujenga utamaduni wa kutafuta taarifa za tasnia kutoka vyanzo vya kuaminika ili kujiepusha na usambazaji wa taarifa potofu zinazoweza kuwa na athari hasi kwenye jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kukuza sekta ya uchukuzi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news