DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kupata elimu hiyo na kuwaandaa kuwa watu wema.


Ametoa wito huo leo Jumapili Februari 23, 2025 alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za Kuhifadhi Qurani Tukufu yanayofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amehimiza madhehebu yote ya dini kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na utulivu hasa katika kipindi cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa yanatoa nafasi ya kujenga maadili bora ikiwemo uaminifu, umakini, na kujitolea. “Washiriki wanajifunza umoja, upendo na mshikamano na wengine kwa ufanisi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mashindano hayo yanahamasisha jamii ya Kiislamu duniani kote kuwa na utamaduni wa kujisomea na kuhifadhi Qur'aan Tukufu. “Hii inachangia kuendeleza utamaduni wa kuheshimu dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii”.


“Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya na taasisi mbalimbali katika kukuza na kuhamasisha shughuli za kidini”.