Gavana wa BoT aongoza uzinduzi wa Ripoti ya Ufuatiliaji wa Fedha zinazoingia kutoka Diaspora

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ameongoza uzinduzi wa Ripoti ya Ufuatiliaji wa Fedha zinazoingia katika nchi kutoka kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni (Cross-border Remittance Diagnostic) katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Ripoti hiyo, Gavana Tutuba amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kwa msaada wake wa kiufundi katika kufanya utafiti huo ambao una mchango mkubwa katika kustawisha sekta ya fedha nchini.
"Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa UNCDF kwa msaada wa kiufundi walioutoa ambao ulisaidia katika katika utafiti huu, ambao ripoti yake inazinduliwa leo. Pia, ninashukuru sana kwa wadau wote wa sekta ya fedha walioshiriki katika utafiti huu zikiwemo wizara na mashirika ya umma, mabenki, watoa huduma za mitandao ya simu, watoa huduma za malipo kwa niia kielektroniki, na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha,” amesema Gavana Tutuba.

Aidha, amesisitiza kuwa fedha hizi zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kufadhili maendeleo ya muda mrefu kupitia majukwaa mbalimbali ya uwekezaji, kubadilishana uzoefu na teknolojia, kuboresha mapato ya kaya, na kusaidia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa michango hii inaunga mkono moja kwa moja Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Tanzania, hasa katika kupambana na umaskini, njaa, kuboresha huduma za afya, elimu bora, maji safi na salama, ajira, ukuaji wa uchumi pamoja na kuleta usawa.

Pia, ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali za kisera ili kuhamasisha malipo ya fedha zinazoingia nchini kupitia waishio ughaibuni zikiwemo kuanzishwa kwa Mfumo ya Malipo ya Kielektroniki ya Mipaka (Cross-border Payment System) kwa lengo la kuunganisha mifumo ya malipo nchini na mifumo ya malipo ya kimataifa na kikanda, na mabadiliko makubwa katika kanuni, kama vile Kanuni za Akaunti za Nje za 2022 (Foreign Account Regulations, 2022) ambayo zimewaruhusu Watanzania waishio nje kuwekeza katika dhamana za serikali.

Gavana Tutuba ameongeza kuwa kuanzishwa kwa masharti ya nyaraka mbadala za kumtambua mteja (Know Your Customer (KYC)) mnamo Machi 2023, kunarahisisha mchakato wa diaspora kufungua akaunti na kushiriki katika mfumo wa kifedha nchini.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe kutoka UNCDF, Bi. Ivana Damjanov, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kusimamia vizuri sekta ya fedha ambayo imepelekea ustawi wa huduma jumuishi za fedha akieleza namna UNCDF ilivyofurahishwa na maendeleo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news