MWANZA-Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Bugando,Dkt.Fabian A.Massaga ameipongeza idara ya Saratani kwa kufanikisha maadhimisho ya siku ya Saratani na kutoa huduma za upimaji bure kwa wananchi wa Mwanza na kusema kuwa Hospitali ya Bugando inahudumia wagonjwa 2,000 wapya kwa mwaka na kati ya hao 80% ya wagonjwa hufika Hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huu.
Dkt.Massaga ametoa takwimu ya ugonjwa wa Saratani kwa Dunia nzima ambapo kwa mwaka watu wanaogundulika na saratani ni 19,000,000 na watu 10,000,000 hufariki kwa ugonjwa huu ndani ya mwaka mmoja.
Tatizo la saratani ni kubwa na ugonjwa huu unaongezeka kwa kasi sana.Kwa Tanzania watu 45,000 hugundulika kuwa na saratani na kati ya hao watu 29,000 hufariki.
Saratani za mlango wa kizazi,matiti, tezi dume na umio zimekuwa ni saratani zinazowapata zaidi Wananchi wa Tanzania, na vitu vinavyochochea ongezeko la saratani hizi ni matumizi ya tumbaku,unywaji wa pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi pamoja na kuchelewa kupata matibabu kitu kinachopelekea mgonjwa wa saratani kufariki.
Serikali yetu imekuwa ikiongeza juhudi za kutatua tatizo hili kwa kutoa chanjo ya HPV kwa wasichana ili kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na kampeni za uchunguzi wa saratani mbalimbali.
Dkt.Massaga ameongeza kwa kusema kuwa Bugando inaendelea kutoa elimu kwa jamii inayolenga kuongeza uelewa wa ugonjwa wa saratani na umuhimu wa kufanya uchunguzi mapema.
"Bugando tunahakikisha wagonjwa wanapata huduma za kibingwa bobezi za saratani ikiwa ni pamoja na vipimo vya maabara ya patholojia,huduma za radiolojia ili kuchunguza hatua ya saratani, upatikanaji wa dawa kemikali pamoja na mashine za mionzi Tiba katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa Saratani,"amesema Dkt.Massaga.
Hata hivyo Dkt.Massaga ameongeza kwa kusema Bugando Health Marathon msimu wa kwanza imekuwa chachu katika kutoa elimu, kufanya mazoezi na kuboresha huduma za saratani.Amewashukuru wananchi wote walioshiriki katika mbio hizo kwani Michango na pesa zimewasaidia sana wagonjwa wa saratani,
Mkurugenzi mkuu ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono wagonjwa wa Saratani kwa kushiriki mbio za Bugando Health Marathon msimu wa pili zitakazofanyika mapema mwezi Agosti, 2025.
Naye Dkt.Heronima Kashaigili amesema kuwa idara ya saratani imekua kwa kiasi kikubwa kwakuongezeka huduma,majengo, mashine pamoja na vifaa tiba ili kuweza kuwahudumia wananchi wa Kanda ya ziwa na viunga vyake wenye ugonjwa wa saratani.
Idara ya Saratani imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo elimu, uchunguzi wa awali wa saratani mbalimbali, Uchunguzi wa kuhakiki Saratani,tiba ya kemikali ya mionzi,tiba shufaa nk.
Dr.Kashaigili amesema,idara ya Saratani imekuwa ikipata wagonjwa wakiwa wamechelewa kufika Hospitali huku ugonjwa ukiwa umesambaa zaidi hali inayopunguza ufanisi wa matibabu na kumuongezea mgonjwa uhitaji wa matibabu yenye gharama kubwa zaidi na ya muda mrefu.
Mwalimu Nyanjura Kakwimba ambaye ni shujaa wa Saratani ya matiti amewaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati wa kupatiwa matibabu na kufuata ushauri wa madaktari kwani Saratani inatibika ukiwahi mapema kupata matibabu.
Aidha, mzazi wa mtoto ambaye ni shujaa wa saratani Bw.Saimon Sinkala amepongeza uongozi kwa jitihada kubwa inayoweka kwa watoto wenye saratani na ametoa rai kwa wananchi wote kuwahi Hospitali na kupata matibabu na si kukimbilia dawa za kienyeji.