Kamati ya Bunge yaipongeza Rufiji kwa utekelezaji bora wa miradi

PWANI-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Rufiji, hususan ukarabati wa Hospitali ya Wilaya pamoja na miradi mingine ya afya, elimu, miundombinu na masoko.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga ameyasema hayo atika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, soko, jengo la utawala na miundominu ya barabara za TARURA inayotekelezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mhe. Nyamoga amepongeza usimamizi mzuri wa miradi hiyo, akibainisha kuwa Rufiji imeonyesha mfano bora wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Mhe. Waziri, tumejionea kazi nzuri ya ukarabati wa hospitali ya Wilaya ya Rufiji. Tumefurahishwa na ubora wa mradi huu, hivyo tunakupongeza kwa usimamizi mzuri. Rufiji ni mfano wa kuigwa," amesema Mhe. Nyamoga.

Aidha, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Salome Makamba, ameeleza kuwa licha ya hospitali hiyo kujengwa mwaka 1963, ukarabati wake umefanyika kwa kiwango cha hali ya juu, jambo linaloonyesha utekelezaji mzuri wa miradi ya serikali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu), Mhe. Zainab Katimba, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imewekeza zaidi ya Sh.Trilioni 1.2 katika sekta ya afya, huku Rufiji pekee ikinufaika na uwekezaji wa Sh.Bilioni 8.3.

Mbunge wa Jimbo la Rufiji, ambaye pia ni Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameeleza kuwa pamoja na maboresho ya huduma za afya, Rufiji inaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari, kiwanda cha ndizi kinachotarajiwa kutoa ajira zaidi ya 8,000, pamoja na ujenzi wa bandari ndogo ya Muhoro kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za kilimo.
Ziara ya Kamati hiyo wilayani Rufiji ilihitimishwa kwa ukaguzi wa miradi mbalimbali, ikiwamo soko la Umwe, jengo la Halmashauri ya Mji, barabara za TARURA, na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Pwani ya Bibi Titi Mohamed.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news