Kamati ya Bunge yaridhishwa na ujenzi Mradi wa Soko la Kariakoo

DAR-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na ujenzi unaoendelea wa Mradi wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Februari 21, 2025 mara baada ya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Mradi wa Soko la Kariakoo pamoja na kujionea eneo lilipotokea tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Florent Kyombo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ilivyopambana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha inaokoa watu na mali wakati yalipotokea maafa nchini.

Makamu Mwenyekiti huyo ameleza kuwa kuanza kwa ujenzi wa mradi wa soko la Kariakoo ni hatua nzuri ambayo itasaidia wafanyabiashara na wengine wanaopata huduma katika eneo hilo kufanya shughuli zao katika eneo rafiki na salama.
Akizungumza kuhusu jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo amesema Serikali imeendelea kuratibu vyema masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuchukua hatua za haraka katika kunusuru uhai na mali za watu wake pindi maafa yanapotokea.

“Tunaendelea kuishukuru na kuipongeza Serikali kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa na moyo wa kujali aliouonesha wakati wote tulipopatwa na haya maafa hadi sasa Serikali inapoendelea kuimarisha miundombinu na kurejesha hali,”amesema Mhe. Kyombo.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa uamuzi wake wa kutembelea na kujionea athari zilizotokana na kuanguka kwa ghorofa hilo na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa Soko la Kariakoo.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake tangu maafa haya yalipotokea hadi sasa katika hatua zote za uokoaji wa watu na mali zao.

"Pia niwapongeze vyombo vya ulinzi na Watanzania wote kwa ushirikiano wote waliouonesha wakati wote wa maafa yalipotokea hadi kufikia hapa Serikali inapoendelea kufanya kila jitihada za kurejesha hali,”alipongeza Mhe. Nderiananga.
Ikumbukwe Ghorofa hilo liliporomoka mnamo tarehe 16 Novemba, 2024 muda wa saa tatu asubuhi katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala, Kata ya Kariakoo, Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Barabara ya Mchikichi Kiwanja Na. 12 Kitalu Na.7.

Jengo hilo, lililokuwa likitumika kwa shughuli za kibiashara ikiwemo maduka na maghala ya kuhifadhi bidhaa za wafanyabiashara. Tukio hilo lilisababisha Vifo vya watu 31 na kujeruhi watu 71.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news