Kuna faida lukuki za kutumia Shilingi ya Tanzania katika huduma na malipo nchini-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kusisitiza kuwa,kupokea malipo kwa fedha za kigeni au kukataa malipo kwa shilingi ya Tanzania ni kinyume cha sheria.

Hayo yamebainishwa leo Februari 26,2025 na Mchumi kutoka Kurugenzi ya Uchumi, Sera na Utafiti wa BoT,Dominick Mwita katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam,Ruvuma na Zanzibar.

Mwita alikuwa akiwasilisha wasilisho kuhusu umuhimu wa matumizi ya Shilingi ya Tanzania katika shughuli za uchumi nchini. Amebainisha kuwa,katazo la kwanza lilitangazwa na BoT mwaka 2007, 2017 na 2023.

Amesema,Serikali kupitia Waziri wa Fedha ilitoa msisitizo kuanzia Julai 1,2024 malipo yote na bei zipangwe na kutangazwa kwa shilingi.

"Kwa hiyo, malipo yote yanayofanyika ndani ya Tanzania ni lazima yafanyike kwa shilingi ikiwa ni pamoja na wageni wanaokuja nchini."

Mwita ameongeza kuwa, "Serikali tayari imeanza utekelezaji, tozo za TANAPA ni kwa shilingi ingawa sheria haikatazi kumiliki akaunti ya fedha za kigeni."
Pia, amebainisha kuwa, Serikali inaandaa mwongozo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini.

Wakati huo huo amesema kuwa, BoT ndiyo yenye mamlaka ya kuchapisha na kusambaza fedha za Tanzania.

"Na sheria inataka bei zote zipangwe na kutangazwa kwa shilingi mfano ada za shule, kodi za nyumba na nyinginezo."

Vilevile, Mwita amebainisha kuwa, miongoni mwa faida za kutumia shilingi kufanya malipo ni pamoja na kuwa na Sera Huru ya Fedha.

Amesema, ni kwa sababu Benki Kuu inahitaji udhibiti wa kiasi cha fedha kilichopo kwenye mzunguko ili kudhibiti mfumuko wa bei.

"Kwa hiyo, kutumia fedha za kigeni ni kuipa nchi nyingine mamlaka juu ya uchumi wetu."

Pia, amesema inasaidia katika ufanisi wa Sera ya Fedha, kwani matumizi makubwa ya fedha za kigeni hudhoofisha ufanisi wa sera hiyo inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei.

Mwita amesema, faida nyingine inayotokana na kuwa na shilingi ni nchi kuwa na faida inayotokana na kuwa na pesa yake yenyewe inayochagizwa na watu kutumia sarafu ya nchi husika.

"Katika mazingira ambayo sarafu ya kigeni ndiyo inayotumika zaidi, faida hiyo huenda kwa nchi ya kigeni."
Mbali na hayo amesema kuwa,kutumia shilingi hupunguza mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni ambayo huleta changamoto ya ya upatikanaji kwa shughuli za kuagiza bidhaa nje ya nchi.

Faida nyingine amesema, ni kudhibiti Sekta ya Fedha. "Kwani, kupungua kwa faida ya nchi kuwa na sarafu yake yenyewe kunaweza kupunguza uwezo wa Benki Kuu wa kuzikopesha benki za biashara ili kuhakikisha uwepo wa uthabiti wa Sekta ya Fedha."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news