NA CHRISTOPHER MSAGATI
Mahakama Manyara
MAHAKIMU wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wameelekezwa kuzingatia utekelezaji wa malengo yanayowekwa na Viongozi wa Mahakama Kitaifa pamoja na Kanda ili kuhakikisha jukumu la Utoaji Haki kwa wakati linatimia ipasavyo..
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akizungumza jambo wakati wa Kikao kazi kilichofanyika Mahakama Kuu Manyara tarehe 24/02/2025.
Hayo yamesemwa jana tarehe 24 Februari, 2025 na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Manyara. Lengo la kikao kazi hicho lilikuwa kufanya tathmini ya Utendaji kazi wa mwaka 2024 na kuweka mipango na matarajio mapya kwa mwaka 2025.
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa Mwihambi akichangia mada wakati wa kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Aidha, Mhe. Kamuzora alisisitiza kwa Mahakimu wote kuhakikisha kwamba, wanazingatia muda wa kumaliza mashauri ambao umewekwa na Uongozi wa Kanda.
“Sote tunajua kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara tumejiwekea malengo ya kumaliza mashauri yanayofunguliwa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pamoja na Mahakama za Wilaya ndani ya miezi sita, aidha kwa Mahakama za Mwanzo tumeweka Malengo ya kumaliza mashauri hayo ndani ya miezi mitatu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anajitahidi kufanikisha malengo hayo ili wananchi hawa tunaowahudumia wazidi kuwa na imani na Mahakama yetu,” alisema Mhe. Kamuzora..JPG)
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo akitoa taarifa ya Utendaji kazi kwa Mwaka 2024 katika kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Akichangia katika taarifa iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo. Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Nenelwa Mwihambi alipongeza juhudi zilizofanywa katika mwaka 2024 kwa kuwa hapakuwa na mashauri ya mlundikano katika Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama zote za Wilaya pamoja na Mahakama zote za Mwanzo zilizopo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa (wa kwanza kulia) pamoja Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu Mhe. Johari Kijuwile wakifuatilia matukio katika kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara wakifuatilia mafunzo ya Elimu ya Afya ya akili kabla ya kuanza kwa kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara.
“Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kwa kweli mnastahili pongezi kwa kuwa tumemaliza mwaka 2024 pasipo kuwa na mashauri ya mlundikano, nawasihi tuendelee na moyo huu kwa mwaka 2025,” alisema Mhe. Mwihambi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto Mhe. Boniface Lihamwike akichangia mada wakati wa kikao kazi cha Mahakimu na viongozi wengine wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Bi. Nyanzobe Magambo Hemedi, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa Maafisa Mahakama hao Kanda ya Manyara kwa kuhakikisha anafuatilia upatikanaji wa watumishi, ukamilishaji wa miradi ya ujenzi pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi ili kufanikisha kazi zinafanyika bila usumbufu wowote.
Katika upande mwingine, Majaji, Naibu Msajili, Mahakimu wa Ngazi zote, Mtendaji wa Mahakama, Mafisa Utumishi na Tawala, Wakuu wa Vitengo kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara na Watumishi wengine waliopo katika jengo la Mahakama Kuu Manyara walipata fursa ya kupata Elimu inayohusu Afya ya Akili kutoka kwa wataalamu wa Hospitali ya Mkoa wa Manyara Dkt. Karim Mbonde na Dkt. Noel Nywelo. Zoezi hili la utoaji elimu hiyo lilifanyika kabla ya kufanyika kikao kazi hicho.