DAR-Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana jijini Dar es Salaa katika Mkutano wa Kamati ya Siasa na Diplomasia ya Jumuiya hiyo (Inter- State Politics and Diplomacy Committee – ISPDC) unaofanyika tarehe 25 hadi 26 Februari, 2025.
Mkutano huo umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Akifungua kikao hicho Balozi Shelukindo amemshukuru Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliyemaliza muda wake Jamhuri ya Zambia kwa uongozi mahiri na wa mfano katika muda wake aliohudumu na kwamba yote yaliyotekelezwa yaliwezekana kufuatia miongozo imara na uratibu makini wa Sekretarieti ya SADC.
Alifafanua kuwa kikao hicho kinatoa fursa ya kupia hatua za utekelezaji za majukumu mbalimbali ya kamati hiyo ikiwa ni pamoja na kujadili uimara wa demokrasia na utawala bora katika uangalizi wa uchaguzi ili kuleta uwazi na umadhubuti katika mchakato wa Uchaguzi mkuu katika kanda.
‘’Pongezi kwa Jamhuri ya Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana. Mafanikio haya ni ishara ya kupevuka kisisasa, ustahimilivu miongoni mwa washindani na ujenzi wa taasisi imara za kidemokrasia’’ alisisitiza Balozi Shelukindo.
Aidha, amezitakia maandalizi mema ya uchaguzi nchi zote zinazojiandaa kufanya uchaguzi mwaka huu ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza utayari wa kushirikiana katika kuendeleza amani, utulivu na utawala bora.
Vilevile, ameeleza maumivu ya kikanda juu ya changamoto wanazozipitia wananchi katika Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mgogoro unaoendelea na kusababisha watu kupoteza maisha na kukosekana kwa makazi.
Hivyo, Mkutano wa pamoja wa Wakuu wa Nchi wa EAC-SADC uliofanyika tarehe 8 Februari, 2025 Dar es Salaam, Tanzania umekaribisha jitihada za kikanda katika kumaliza changamoto ya mgogoro wa DRC na pia ulisisitiza umuhimu wa usuluhishi kwa njia za kidiplomasia ili kuunganisha mchakato wa amani wa Luanda na Nairobi. Hatua hii inaonesha nia thabiti ya Afrika kutafuta ufumbuzi katika kumaliza changamoto zake.
Kadhalika, Balozi Shelukindo amezipongeza nchi wanachama na Sekretarieti ya SADC kwa kufanikisha ufunguzi wa Mtandao wa Wanawake wa Utatuzi wa Migogoro katika Kanda ya SADC uliofanyika tarehe 28 Januari, 2025 ambapo hatua hiyo italeta ujumuishi na kutambua nafasi yao katika utatuzi wa migogoro pamoja na kuwa chachu ya kupeleka mbele nafasi ya mwanamke katika ujenzi wa amani na sauti zao kusikilizwa.
Pamoja na masuala mengine mkutano huo utapitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mageuzi zinazoendelea katika ufalme wa Lesotho, Utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (MCO), Baraza la Mawaziri, na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali na utekelezaji wa mapendekezo ya Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi (SEOMs).