SHARJAH-Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe.Mama Mariam Mwinyi amewasili Sharjah kwa ziara na kupokelewa na Mke wa Kiongozi wa nchi hiyo, Sheikha Jawaher bint Mohammed Al Qasimi, katika Ikulu ya Al Badi nchini humo.
Ziara hiyo inalenga kubaini fursa za maendeleo ya kijamii zilizomo nchini humo zinazozingatia kujenga uwezo na uwezeshaji wa maendeleo yenye tija kwa umma.

Halikadhalilka majadiliano hayo yalijikita kuwekeza katika mustakabali wa jamii kwa wanawake na vijana, ujuzi na maarifa muhimu kuimarisha mshikamano wa familia na kuzingatia maadili na utamaduni.
Mke huyo wa Kiongozi wa Sharjah amempongeza Mama Mariam Mwinyi kwa juhudi anazochukuwa kwa Maendeleo ya Zanzibar na kuunga mkono makundi ya kijamii hususani Vijana na Wanawake.
Mwaka 2024, Sheikha Jawaher bint Mohammed Al Qasimi, aliitembelea Zanzibar na kukutana na Mama Mariam Mwinyi na kupanga Mipango ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa ajili ya kuimarisha Ujuzi wa Wanawake na Vijana kwa kutumia Rasilimali za ndani kwa ajili ya Maendeleo endelevu ya Zanzibar.