KILIMANJARO-Manispaa ya Moshi imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, ikiongeza mapato kutoka bilioni 6.1 mwaka 2021 hadi bilioni 9.9 mwaka 2025, ongezeko la takribani bilioni 3.7.
Mafanikio haya yanatajwa kuwa matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa ili kuboresha vyanzo vya mapato na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Akizungumza katika kikao cha bajeti cha mwaka wa fedha 2025/26, Meya wa Manispaa ya Moshi Zuberi Kidumo amesema kuwa ongezeko hilo limechangiwa na mbinu mpya za ukusanyaji wa mapato pamoja na uwekezaji katika miradi yenye tija.
"Tumeimarisha mifumo yetu ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia teknolojia ya kisasa, tumeongeza uwazi katika makusanyo, na pia tumewekeza katika miradi inayozalisha kipato kwa manispaa. Hatua hizi zimechangia ongezeko kubwa la mapato," alisema Zuberi Kidumo.