ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezisisitiza jumuiya za Chama Cha Mapinduzi kuwahamasisha wanachama na wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili CCM ishinde kwa kishindo.

Dkt.Mwinyi amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya Wana CCM kutojitokeza kupiga kura wakati wa Uchaguzi jambo linaloipunguzia Kura za Ushindi Chama hicho.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza UWT kwa kazi nzuri walioifanya ya uhamasishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuiagiza kuendelea na mwamko huo.
Halikadhalika Dkt.Mwinyi amewapongeza na kuwakaribisha wanachama 2,439 wa Chama cha ACT Wazalendo kwa uamuzi wa kujiunga na CCM kwani wamefanya uamuzi sahihi na kuwaahidi ushirikiano wa kiwango cha juu.
Amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiendesha nchi kwa mafanikio na kudumisha amani.

Hatimaye alizungumza na wazee wa CCM Afisi ndogo ya Chama Cha Mapinduzi Chakechake na baadae msafara huo ukaelekea katika Mkutano na Wanachama Mauwani Kiwani ambapo wana CCM walijipanga barabarani kumlaki Dkt. Mwinyi.