MARA-Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya leo ameiongoza Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara kukagua eneo lilalotarajiwa kujengwa nyumba ya kupumzikia viongozi (rest house) katika eneo la Bweri, Manispaa ya Musoma.
Akizungumza baada ya kupokea maelezo ya wataalamu na kukagua eneo hilo, Bwana Kusaya amewataka wataalamu wanaohusika na ujenzi wa mradi huo kuyachukua maoni yaliyotolewa na Kamati ya Usalama wa Mkoa na kuyafayia kazi kwa haraka.
“Maoni yaliyotolewa na viongozi hapa na yatakayotolewa baadaye yazingatiwe katika mchoro wakati maeneo halisi majengo yatakayojegwa yanaangaliwa ili kuboresha mchoro uliopo sasa,” amesema Bwana Kusaya.
Aidha, Bwana Kusaya amewataka wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa kuendelea kuifikiria michoro ya nyumba hiyo na kama watapata maoni zaidi ya kuboresha wayawasilishe kabla ya ujenzi wa kituo hicho haujaanza ili kuboresha mradi huo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandishi Richard Moshi amesema michoro ya majengo hayo imeandaliwa na wataalamu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na itakuwa na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya mahitaji ya sehemu za kupumzikia viongozi.
Mhandisi Moshi amesema ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 na tayari maandalizi muhimu ya mradi huo yamefanyika ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti na kuandaa michoro na kufanya ukadiriaji majenzi ya mradi huo.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mara Arch. Celestine Kaitaba amesema majengo matano yanatarajiwa kujengwa katika nyumba hiyo ya kupumzikia viongozi.
Arch. Kaitaba amesema michoro ya majengo hayo imezingatia ramani za majengo ya kupumzikia viongozi pamoja na uhalisia wa eneo lenyewe la mradi.

Katika ziara hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Mara ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na baadhi ya watumishi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mara.