KILIMANJARO-Mkurugenzi wa Hospitali ya Kibong'oto, Dkt. Leonard Subi ameiomba Wizara ya Madini na wadau kuweka juhudi za makusudi ili kuzuia uzalishaji wa vumbi la Silicosis kwenye shughuli za uchimbaji hususan katika machimbo ya Tanzanite Mirerani kwa kuwa ugonjwa huo unaweza kuzuilika.

Aliyasema hayo Februari 13, 2025 Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara fupi ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo aliyeitembelea hospitali hiyo iliyopo Wilaya ya Siha kujionea hali halisi ya athari za ugonjwa wa TB na Silicosis uliowaathiri wachimbaji wadogo wa madini hususan wanaofanya shughuli zao katika migodi ya Tanzanite, Mirerani.
Alieleza kwamba, takriban wagonjwa 2—25 walioko katika wodi wanapatiwa oksijeni kila siku inayogharimu Dola za Marekani 220,000 kwa mwaka sawa na shilingi milioni 500.
Vilevile, Dkt. Subi ilieleza kuwa kati ya wagonjwa 45 waliofariki hospitalini hapo mwaka 2023, vifo vyao vilitokana na magonjwa ya TB na Silicosis.
‘’Kutokana na hali hiyo, wagonjwa hawawezi kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa ajili ya ustawi wa familia zao na badala yake wanageuka kuwa wategemezi,’’ alisema Dkt. Subi.
Katika hatua nyingine, Mbibo alipokea taarifa ya mwenendo wa makusanyo ya maduhuli ya madini katika mkoa wa Kilimanjaro kutoka Kwa Afisa Madini Mkazi Abel Malulu ambaye alisema hadi kufikia Novemba 30, 2024, ofisi hiyo ilikuwa imekusanya jumla ya shilingi 2,251,511,496.79 sawa na asilimia 110.2 ya lengo kwa kipindi cha Julai hadi Januari, 2025.
Malulu aliongeza kwamba, kwa mwaka wa Fedha 2024/25, ofisi ya madini Kilimanjaro ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 3,500,000,000/- sawa na shilingi 291,666,666.67 kwa mwezi.
‘’Naibu Katibu Mkuu, mafanikio ya makusanyo yanategemea sana vyanzo vikuu ambavyo ni ada za leseni, maduhuli katika madini yanayozalishwa na tozo nyingine kama vibali,’’ alisema Malulu.
Pamoja na kueleza mafanikio hayo, Malulu alisema mkoa huo umejiwekea mikakati mbalimbali ya kufikia malengo ikiwemo kufuatilia kwa kina miradi ya ujenzi wa barabara hususan iliyo chini ya TARURA na TANROAD ikiwa ni pamoja na kuifanyia ukaguzi ili kupata uhakiki wa malipo stahiki ya maduhuli, ukaguzi na usimamizi wa Baruti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ukataji wa vibali husika na kutatua changamoto za wawekezaji ili waweze kuongeza uzalishaji na kufuatilia miradi.