DODOMA-Mkurugenzi Mtendaji wa lebo ya WCB Wasafi na Wasafi Media, Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) amesema msanii wa lebo hiyo,Mbwana Yusuf Kilungi (Mbosso) sasa anajitegemea ila ataendelea kumuunga mkono kadri itakavyohitajika.
Amesema,wiki mbili nyuma waliongea na Mbosso na aliniomba aanze kujisimamia na amempa baraka zote.
"Na Mbosso ni mdogo wangu, sababu ya kumsaini Mbosso nilikuwa nampenda, mimi na Mbosso hatujawahi kugombana.
"Nikamwambia (Mbosso) kwa jinsi ulivyoniheshimu kwa ulivyonipenda, tulivyopendana siwezi kukutoza hata shilingi 10, kwa hiyo sijamtoza hata shilingi 10, nafikiri tumeshakamilisha vitu vyake ameanza kujisimamia rasmi hata show aliyokuja huku (Dodoma) amekuja rasmi kama show za kujisimamia."
Pia, Diamond Platnumz amesema wao kama familia ya Wasafi wataendelea kumuunga mkono Mbosso.
"Nitampigania na kumlinda sehemu ninayoweza kumlinda, ninamshukuru kwa kutumia hekima, alikuja tayari kwa ajili ya kulipa nikamwambia siwezi kukutoza, kwa heshima na mapenzi aliyonionesha Mbosso kumtoza hela ni aibu."