Mchengerwa awaweka kikaangoni wakurugenzi

DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameagiza tathmini ifanyike kubaini maeneo ambapo wanafunzi wanalazimika kusoma chini au kukaa chini ya miti.
Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wao kuandikiwa barua za kujieleza juu ya hali hiyo.

Agizo hilo limetolewa Februari 13, 2025, jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kukabiliana na msongo wa mawazo kazini kwa watumishi wa TAMISEMI.

Mchengerwa amesisitiza kuwa haiwezekani katika karne hii wanafunzi wakakosa madarasa au madawati, ilhali serikali imetumia matrilioni ya shilingi kuboresha sekta ya elimu.

"Miaka yote tumekuwa tukipata usumbufu ikifika Desemba na Januari, lazima zitafutwe sh. bilioni 250 au 300 kwa madarasa na madawati. Lakini sasa miaka miwili imepita hatujamuomba Rais fedha za kujenga madarasa au kununua madawati. Msisubiri msukumwe, fanyeni kazi," amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Ameagiza Idara ya Usimamizi wa Elimu ya TAMISEMI kufanya tathmini ya shule zote za msingi na sekondari zilizo chakavu ili kuweka mpango wa ukarabati.

Aidha, amewapongeza watumishi wa TAMISEMI kwa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ufanisi na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wananchi.

Kuhusu sekta ya afya, Mchengerwa ameeleza kuwa juhudi za TAMISEMI zimechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku akihimiza ufuatiliaji wa karibu kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Aidha, amewahimiza watumishi hao kufuatiliwa kwa karibu Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya na kwenye vituo vya afya ili waongeze kasi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news