NA JOVINE BISHANGA
Mahakama Kigali
MKUTANO wa Tatu wa Mwaka wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (the East African Court of Justice) unaowaleta viongozi mbalimbali wa Mahakama katika nchi hizo umeanza leo tarehe 18 Februari, 2025 nchini Rwanda kujadili mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za utoaji haki kwenye ukanda huo.
Kutoka kushoto kuelekea kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi Dar es Salaam, Mhe. Zahra Abdallah Maruma, Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Bokobora Masara, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Lazaro Londo, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovine Costantine Bishanga.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wanaoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, ambaye amemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wamehudhuria ufunguzi wa Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika hoteli ya Marriott iliyopo jijini hapa.
Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki Mkutano huo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi Dar es Salaam, Mhe. Zahra Abdallah Maruma, ambaye atamwakilisha Mhe. Prof. Juma katika jopo la Majaji Wakuu watakaojadili na kuhimiza namna bora ya kutatua migogoro kwa njia mbadala (alternative dispute resolution).
Kwa upande mwingine, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Bokobora Masara, wanashiriki pia katika Mkutano huo muhimu.

Kadhalika, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovine Costantine Bishanga ni miongoni mwa Viongozi wa Mahakama kutoka Tanzania wanaohudhuria Mkutano huo.
Mkutano huo wenye kauli mbiu “Justice, Ethics and Enforcement of Decisions: A Judicial Pathway for Regional Development” umefunguliwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Mukantaganzwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame, ambaye amehimiza wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Afrika Mashariki pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili.
Mbali na kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, Mkutano huo pia utajadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya Akili Mnemba “Artificial Intelligent” katika shughuli za Mahakama, sambamba na wajibu wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kushughulikia mashauri ya haki za binadamu na kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Jaji Zahra Maruma (juu na chini) akiwa kwenye jopo la Majaji Wakuu wakijadili namna bora ya kutatua migogoro kwa njia mbadala (ADR).
Wadau mbalimbali wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Serikali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Lazaro Londo, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Stephen Mbundi, nao wanahudhuria Mkutano huo.