NA MARY GWERA
Mahakama Dodoma
UJUMBE kutoka Benki ya Dunia (WB) umekiri kuwa mpaka sasa Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama kwa wananchi unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa miradi bora kuwahi kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akisalimiana na Afisa kutoka Benki ya Dunia, Bi. Donna Andrew leo tarehe 24 Februari, 2025 Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma. Bi. Donna pamoja na wenzake wameanza ziara ya kuangalia hatua ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kiongozi wa Ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour akizungumza wakati wa kikao kati ya ujumbe huo ambao umeanza ziara ya kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama kilichofanyika leo tarehe 24 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
Afisa kutoka Benki ya Dunia, Bi. Donna Andrew akipongeza Mahakama kwa utekelezaji mzuri wa Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama katika kikao kati ya Ujumbe kutoka Benki hiyo na Mahakama ya Tanzania kilichofanyika leo tarehe 24 Februari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 24 Februari, 2025 wakati wa kikao kati ya ujumbe huo ambao umeanza ziara ya kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma za Mahakama zinazomlenga mwananchi unaofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Ujumbe huo na wa Mahakama ya Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Kiongozi wa Ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri ya Mradi huo ambao ni moja ya Miradi inayoendelea kufanya vizuri.a.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) akifungua kikao cha majadiliano kati ya ujumbe kutoka Benki ya Dunia na Mahakama ya Tanzania wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka Benki ya Dunia. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma leo tarehe 24 Februari, 2025. Aliyeketi kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
“Mradi huu umetupa uzoefu mzuri kwetu sote na ni moja kati ya miradi inayofanya vizuri, hata hivyo naomba kutoa angalizo kwa Mahakama ya Tanzania kuweka vizuri vipaumbele vilivyobaki ili kuweza kukamilisha kwa wakati kazi zilizobaki kufikia Juni mwaka huu,” amesema Bi. Owour.
Aidha, amesema kuwa lengo la ziara yao ni kufahamu hatua iliyofikiwa katika mradi eneo la ujenzi, TEHAMA na kuangalia namna bora zaidi ya kuwezesha kusogeza mbele kazi zilizobaki ili ifikapo Juni mwaka huu ambapo ndio mwisho wa Mradi huo kila kitu kiwe kimekamilika.
Naye, mmoja wa Wajumbe kutoka Benki ya Dunia, Bi. Donna Andrew amekiri kuwa, Mradi wa Maboresho wa huduma za Mahakama unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania ni moja kati ya Miradi inayofanya vizuri.
“Huu ni moja kati ya Mradi unaofanya vizuri, na hii ilidhihirishwa nah atua ya Benki ya Dunia kuiongezea fedha Mahakama za (additional financing) za kutekeleza miradi ya maboresho ya huduma za Mahakama zinazomlenga mwananchi,” amesema Bi. Donna.
Hali kadhalika, ametoa rai kwa Mahakama ya Tanzania kuelekeza nguvu zake katika miradi iliyobaki iweze kukamilika kufikia mwezi Juni mwaka huu ambao ndio utakuwa mwisho wa Mradi huo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Mgeni Rasmi Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wanaoendelea kuipatia Mahakama unaowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Tunashukuru kwa ushirikiano ambao Benki ya Dunia inaendelea kutoa kwa Mahakama kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ambayo yanaifanya kuwa Mahakama ya mfano na kutembelewa na Mahakama kutoka Uganda, Malawi, Ireland, Zimbabwe, Zanzibar na nyingine kwa lengo la kuja kujifunza na kupata uzoefu kuhusu uboreshaji wa huduma za Mahakama,” amesema Mtendaji Mkuu.
Aidha, Prof. Ole Gabriel ametoa pongezi kwa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama (JDU) kwa kazi kubwa inayofanywa chini ya uongozi wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo hicho, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha kwa kusimamia vema Mradi huo ambao unatarajia kukamilika ifikapo Juni mwaka huu.
Ameongeza kwa kuuahidi ujumbe kutoka Benki ya Dunia kuwa Mahakama itaongeza nguvu zaidi kusimamia miradi inayoendelea ili inapofika mwisho wa Mradi iwe imekamilika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma za Mahakama zinazomlenga mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema kuwa hadi kufikia Desemba, 2024 asilimia 85 ya Viashiria Muhimu vya Utendaji (KPIs) vilikuwa vimefikiwa.
Aidha, Mhe. Dkt. Rumisha amebainisha kuwa jumla ya viashiria 12 kati ya 14 vimefikiwa.
Akizungumzia maendeleo ya Miradi ya Ujenzi ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa vinavyoendelea kujengwa, Jaji Rumisha amesema kuwa baadhi ya majengo ya Mahakama hizo ambazo ni Simiyu, Geita na Njombe yapo katika hatua ukamilishwaji (finishing) huku mengine yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Pamoja na kufanya kikao Ujumbe huo umepata pia fursa ya kutembelea Chumba cha Kutolea Taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) na kupongeza Mahakama kwa hatua nzuri iliyofikiwa ukilinganisha na mara ya mwisho mwaka jana walipokitembelea chumba hicho.
Picha mbalimbali za Wajumbe wa kikao wakifuatilia kinachojiri wakati wa ufunguzi wa kikao cha ujumbe kutoka Benki ya Dunia na Watumishi wa Mahakama kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania.
Meza kuu katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Benki ya Dunia na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar.
Sehemu ya picha za ujumbe kutoka Benki ya Dunia walipotembelea Chumba cha Kutolea Taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) leo tarehe 24 Februari, 2025.(Picha na MARY GWERA, Mahakama).
Katika ziara yao ya wiki moja miongoni mwa shughuli zitakazofanywa na Ujumbe huo ni pamoja na kutembelea na kukagua baadhi miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi ikiwemo Singida, Geita, Simiyu na nyingine na mwisho tarehe 01 Machi, 2025 watahitimisha kwa kufanya majumuisho / maazimio katika kikao kitakachofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke.