PWANI-Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kiwango cha uchangiaji hadi kufikia shilingi bilioni 10 kwenye mfuko mkuu wa serikali kwa mwaka ujao.
Mchechu ametoa wito huo leo Februari 24,2025 katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo uliofanyika katiks Chuo cha Uongozi cha Mwalimu J. Nyerere kilichopo Kibaha mkoni Pwani.
Amesema, kwa sasa mizania ya shirika imeongezeka na kwamba kwa mwaka huu uchangiaji utaongezeka kwa asilimia 300 kutoka bilioni mbili hadi kufikia bilioni 6.5 kwenye mfuko wa serikali nje ya kodi na makusanyo wanayotoa serikalini.
"Shirika limepiga hatua kubwa, hivyo nina tamani kiwango cha uchangia kwenye mfuko wa serikali uongezeke hadi kufikia bilioni 10 kwa mwaka ujao."
Amesema, katika mashirika ambayo kama Ofisi ya Msajili wa Hazina inafurahishwa sana nayo ni NHC kwa kuendelea na utendaji mzuri na mageuzi makubwa wanayoyafanya katika utekelezaji wa miradi.
Aidha,amelitaka shirika hilo mbali na kutekeleza miradi hiyo ni vizuri pia wakajitahidi kuwekeza zaidi kwenye maeneo ambayo yataleta mavuno mengi na kutolea mfano katika mikoa miwili ya Dar es salaam na Dodoma.
"Japo mnaendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini, wekezeni zaidi pia kwenye maeneo ambayo yataleta mavuno mengi kama Dar es salaam na Dodoma," amesema.
Pia Mchechu, ameitaka NHC iangalie kasi ya uendeshaji wa miradi kwa kuwa kuna changamoto kubwa za nyumba na kwamba wajipambanue ili waweze kuwa suruhisho la uhaba wa nyumba.
Aidha, amewataka kuwa na timu yenye umoja na mshikamano ili kuleta mafanikio na kwamba serikali haitashughulika na watu wenye majungu kwa kuwa inataka utendaji kazi wenye tija kwa serikali na wananchi kwa ujumla.
Amesema, NHC ndio tegemeo la watu kuishi kati kati ya miji hivyo watumie mali zao kuongeza miradi na kwamba anatamani miradi ya ubia iendeleee kwa kasi kubwa kwa kuwa ina umuhimu mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo,Bw. Hamad Abdallah alimuomba Msajili wa Hazina kusaidia kuhakikisha kwamba madeni ya kodi ya pango kwa taasisi za serikali na halmashauri yanalipwa ili yaweze kusaidi kufanya miradi kwa wakati.
"Kwa mwaka 2023/2024 kulikuwa na deni la shilingi bilioni 27 na kwa sasa limepungua hadi bilioni 23 na endapo litalitolewa litasaidia kufanya miradi mingine."
Amesema hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu gawio lote litakuwa limelipwa kwa asilimia mia moja na kwamba wataendelea kuongeza hadi kufikia shilingi biloni 10 kwa mwaka ujao.
Aidha,kabla ya mkutano huo, Baraza hilo lilifanya uchaguzi wa Katibu Mkuu na Msaidizi wake watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.

Akitangaza matokeo hayo Kamishina wa Kazi, Zevyanji Silungwe, amesema kuwa jumla ya wajumbe 80 walipiga kura ambapo kati ya kura hizo kura 3 zimeharibika.
Silungwe alimtangaza Faida kuwa Katibu Mkuu aliyepata kura 55 dhidi ya Godlove Godwin aliyepata kura 22 na ndiye atakuwa Katibu Msaidizi.