DAR-Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Khamis Luwonga, maarufu kwa jina la Meshack, adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake, Naomi Marijani.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya mahakama kuridhika kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi, licha ya mawakili wake kudai kuwa alikuwa hana akili timamu wakati wa tukio hilo.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba nne ya mwaka 2019, iliyosikilizwa na Mahakama Kuu, upande wa utetezi ulidai kuwa mshtakiwa alikuwa hana akili timamu wakati wa kutenda kosa hilo.
Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kukamatwa, mshtakiwa alichukuliwa na kufanyiwa vipimo vya uwezo wa kufikiri.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mwenendo wa kesi, ilibainika kuwa mshtakiwa alikuwa na akili timamu kwani aliweza kufikiria na kupanga kutenda matukio yote kwa utaratibu wa kijasusi.
"Mahakama hii imemtia hatiani mshitakiwa kwa kumuua mke wake chini ya kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya adhabu."
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mzava, aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wanaume wengine.
"Kifo cha Naomi kimeonyesha kuambatana na mateso makali na kufanya vijana na watu wengine kuwa na hofu ya kuingia katika ndoa," alisema Mzava akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter.
Mzava pia aliomba mahakama ikabidhi kielelezo namba PW8, ambacho ni mabaki ya mwili wa Naomi, kwa familia yake ili wamzike kwa heshima ya kidini.
Wakati akitoa hukumu, Jaji Mwanga alieleza kuwa kosa la mauaji halina adhabu mbadala zaidi ya hukumu ya kifo.
"Hili ni kosa la mauaji. Mikono yangu imefungwa kwa kiapo changu cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sheria za Tanzania, adhabu ni moja tu,kunyongwa hadi kufa."
"Ninamuhukumu Khamis Luwonga maarufu kwa jina la Meshack adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake Naomi Marijani."
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa Luwonga, ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, anadaiwa kutekeleza mauaji hayo Mei 15, 2019, katika eneo la Gezaulole, Kigamboni. Ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha kuwa Luwonga alimtesa Naomi kabla ya kumuua, na baada ya kifo chake, alizika mwili wake shambani kwa kupandia migomba juu yake ili kuficha ushahidi.
Baada ya hukumu kutolewa, baba mdogo wa marehemu, Robert Marijani, alisema kuwa familia yao imeridhika na uamuzi wa mahakama.
"Mtoto wangu alikuwa mpambanaji, mjasiriamali mchakalikaji, lakini mume wake hakutaka ajishughulishe. Tulipomuwezesha kufanya biashara, ikawa kero kwa mume wake. Kabla ya kifo chake, tulishawahi kuwasuluhisha lakini huwezi kujua akili ya mtu," alisema Marijani.
Aliongeza kuwa,sasa wanatarajia kumzika Naomi upya kwa sababu mwili wake haukuzikwa kiheshima.
"Hatuwezi kumrudishia, kwa sababu yeye aliamua kupandia migomba, na sisi tunataka kuzika rasmi," alisema.
Ndugu wengine walieleza kuwa sasa wanapata nafasi ya kupumzika baada ya miaka kadhaa ya majonzi na mapambano ya kutafuta haki.
"Tumekuwa tukilia kila siku tukiomba haki ipatikane ili tumzike Naomi kwa heshima," alisema mmoja wa ndugu.
Hukumu hii inahitimisha kesi iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu na jamii, huku wengi wakilitazama tukio hilo kama onyo dhidi ya ukatili wa kijinsia.