DAR-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Wataalamu kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), waliomtembelea kwa lengo la kujitambulisha na kumjulisha kuhusu maendeleo ya mradi huo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekutana na Ujumbe huo Ofisini kwake Kivukoni jijini Dar es Salaam, tarehe 24 Februari, 2025.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kisheria ili kuharakisha na kurahisisha utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki.
“Sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunawaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha katika maeneo mbalimbali ya kisheria ili muweze kukamilisha mradi huu.”
Awali, Meneja wa Sheria wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, Bw. Stanley Mabiti, akizungumza kuhusu kikao hicho, amesema kuwa kikao baina ya wataalamu hao na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kwa ajili ya kujitambulisha na kumfahamisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu maendeleo ya mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia ishirini na tatu.
Katika hatua nyingine Bw. Mabiti ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika masuala yanayohusu Mikataba na Sheria kwa ujumla kwenye utekelezaji wa Mradi huo.
“Tunaishukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwani imekuwa ikitupatia ushikiano wa kutosha, hivyo kurahisisha utekelezaji wa mradi huu.”
Ujumbe huo kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki uliongozwa na Meneja wa Sheria, Bw. Stanley Mabiti ambaye aliongozana na Washauri wa Sheria wa Mradi huo, Bw. Yohana Mganga na Bi. Mectrida Rweyemamu.