NEW YORK-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amehudhuria Mkutano na kikao kazi cha kujadili na kuleta mageuzi ya mfumo wa kutatua migogoro kati ya mataifa ya Afrika na wawekezaji (Investor State Dispute Settlement-ISDS), mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, nchini Marekani tarehe 17 Februari, 2025.

Mkutano huo umeyakutanisha mataifa yenye Makampuni ya uwekezaji duniani na mataifa yenye rasilimali kwa ajili ya kujadili rasimu ya Sheria za Miongozo ya Mikataba ya Uwekezaji baina ya Wawekezaji na mataifa yenye rasilimali, ambapo Sheria hiyo itatumika kutatua changamoto za migogoro ya uwekezaji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa mataifa mengi yaliyoendelea yamebadilisha mifumo yao ya sheria na kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kuleta ufanisi na tija katika uwekezaji.
“Mataifa mengi makubwa duniani yamefanya maboresho mengi kwenye sekta ya sheria ili kuendana na ukuaji wa teknolojia duniani.”
Aidha, Mhe. Johari amesema kuwa ipo haja ya Tanzania kufanya maboresho kwenye Sheria ziweze kuleta ufanisi katika uchumi shindani wa kidunia ambayo hatima yake huamuliwa na mikutano hiyo.
“Tanzania pia haiwezi kubaki nyuma lazima ishiriki na kuona ni namna gani inaweza kunufaika na majadiliano haya ambayo ni muhimu kwa ukuaji na ustawi wa uchumi wetu.”