Mwanza waipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwasogeza huduma za kisheria karibu

MWANZA-Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma za Kisheria karibu zaidi na wananchi kupitia Kliniki ya Sheria bila malipo iliyofanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Mwanza.
Wananchi hao wametoa maoni yao wakati wa kilele cha kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza iliyoanza tarehe 17 na ambayo inakamilika tarehe 23 Februari ,2025 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Jijini Mwanza.

Akizungumzia kuhusu mwitikio wa Kliniki hiyo Wakili Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Silinde Gumada amesema wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za ushauri wa kisheria katika Kliniki hiyo ambapo wengi wao walikuwa na changamoto katika maeneo ya migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa, ajira na mirathi.
“Kliniki hii ya ushauri wa kisheria hapa Mwanza imekuwa na mafanikio makubwa kwani wananchi wengi wamejitokeza na mawakili wetu wameweza kuzitatua kero za wananchi hao, masuala ya ardhi, ajira, ndoa na mirathi yalijitokeza zaidi.”

Aidha, Bw. Silinde alitoa wito kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Mwanza kuendelea kuwasikiliza wananchi kwa kuwatembelea kwenye maeneo yao wanayoishi na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria wanazokumbana nazo wananchi hao.

“Niwaombe Kamati ya Mkoa kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwafikia kwenye maeneo yao wanayoishi na kutoa huduma za ushauri ili wananchi wapate haki zao.”

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya mkoa wa Mwanza, Bi. Samira Manento ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendesha Kliniki hiyo kwa kuwashirikisha Mawakili na Wanasheria kutoka kwenye Taasisi nyingine za Serikali.
"Sisi kama Mawakili kutoka Taasisi tofauti tunamshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutupa fursa hii ya kutoa huduma za ushauri wa kisheria kwa wananchi, pia katika Kliniki hii tumeweza kupokea wananchi wengi na kuwahudumia."

Bi. Fatuma Ally mmoja ya wananchi waliojitokeza na kupata huduma katika Kiniki ya Sheria bila malipo amefurahishwa na huduma aliyoipata kupitia Kliniki hiyo, huku akitoa wito kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali ambayo Kliniki ya Kisheria itafanyika kujitokeza na kupata huduma za ushauri wa kisheria.

“Nawashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja katika mkoa wa Mwanza na kutoa huduma hii bure ambayo imekuwa msaada kwetu sisi watu wenye kipato cha chini.”
Naye Bi. Lucy Linda ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza na kutoa huduma za ushauri wa kisheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa huo, huku akiomba kuongezwa muda wa kufanyika kwa Kliniki hiyo kutoka siku saba za sasa hadi siku kumi na nne ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hiyo.

“Niwapongeze Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutupatia huduma hii imetusaidia sana kupata ufahamu wa kisheria, pia tunatamani muongeze muda kwani wiki moja haitoshi walau mfanye wiki mbili.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news