Mwekezaji Salehe Salim Almamry na Wakili wa Sheki Mfinanga wanakabiliwa na mashtaka 60

MWEKEZAJI wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini, Salehe Salim Almamry, pamoja na wakili wa kujitegemea Sheki Mfinanga, wanakabiliwa na mashtaka 60, yakiwemo utakatishaji wa fedha na uhujumu uchumi, huku upande wa Jamhuri ukitarajia kuwasilisha mashahidi 80 katika kesi hiyo.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ameidhinisha kesi hiyo kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Arusha.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Erasto Philly, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Edga Bantulaki, akisaidiwa na waendesha mashtaka Jackline Mosha na Allawi Miraji, pamoja na Yona Msengi wa TAKUKURU, alieleza kuwa Jamhuri imekamilisha ushahidi na inatarajia kuwasilisha nyaraka 461 za ushahidi wa maandishi pamoja na nyaraka 12 za ushahidi unaoonekana.

Alisema miongoni mwa mashahidi hao ni wafanyabiashara wakubwa waliotumiwa na mtuhumiwa Salehe Almamry kupitia kampuni yake ya Tarangire Sunset Limited kutakatisha fedha.

“Mtuhumiwa Salehe Almamry anadaiwa kutakatisha zaidi ya bilioni 60 baada ya kuwadhulumu wabia wake wawili raia wa Saudi Arabia, Khalid Alraj na Abdulkarim Alraji, katika kampuni ya Tarangire Sunset Limited.”

Aliendelea kufafanua kuwa washtakiwa pia wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka, na kutoa taarifa za uongo kwa mamlaka za kiserikali kwa nia ya kujipatia fedha isivyo halali.

Katika shtaka namba 16, Almamry anadaiwa kughushi nyaraka ikionyesha kuwa wabia wake Abdulkarim Mohamed Alraj na Khalid Alraj walikubali hisa zao za asilimia 18 kuchukuliwa, jambo ambalo si la kweli.

Makosa haya yanadaiwa kufanywa kati ya Machi 2019 na Mei 2024, katika mikoa ya Arusha, Manyara, Pwani, na Dar es Salaam.

Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Mkazi Erasto Philly alisema;

"Mtuhumiwa namba moja Salehe Almamry ataendelea kukaa mahabusu kwa kuwa kesi yake haina dhamana, huku mtuhumiwa namba mbili Sheki Mfinanga akiendelea na dhamana yake hadi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi.

"Mahakama yetu imesikiliza maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika, na sasa tunasubiri taarifa rasmi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu tarehe ya usikilizaji wa kesi hiyo."

Miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri waliotajwa ni mfanyabiashara na mkulima mkubwa Gerald James Milla, Said Iddi Kipingu, wakili John Beatus Kasegenya, Abdull Said Msalaam, Suleiman Nkya, Abdulkareem Mohamed Alraj, Khalid Alraj, na Abano Gilla.

Kesi hiyo sasa inasubiri tarehe rasmi ya kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news