Naibu Waziri Mwinjuma asisitiza ujenzi wa Uwanja wa Arusha kukamilika kwa wakati

ARUSHA-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, amewasisitiza wakandarasi wanaojenga uwanja wa michezo Arusha kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati kabla ya ukaguzi wa mwisho wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kauli hiyo ameitoa Februari 15, 2025, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo unaojengwa katika kata ya Olmoti, jijini Arusha.

Uwanja huo unatarajiwa kutumika katika mashindano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.

“CAF wanakuja kufanya ukaguzi wa mwisho mwezi Julai 2026 na sisi tunataka mradi huu ukamilike mwezi Mei 2026, yaani miezi miwili kabla ya ukaguzi huo,” alisema Mheshimiwa Mwinjuma.
Mheshimiwa Mwinjuma aliongeza kuwa mradi huu ni wa kipaumbele kwa Serikali na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameonesha ujasiri mkubwa katika kuhakikisha uwanja huu unakamilika kwa wakati.

“Mheshimiwa Rais anajua umuhimu wa uwanja huu kukamilika ili tusiwe nyuma kwenye ratiba ya CAF ya kuandaa mashindano ya AFCON 2027. Ndio maana ametuelekeza tufuatilie kwa karibu na kuhakikisha kila kitu kinalipwa kwa wakati,” alisisitiza.

Aidha, Mheshimiwa Mwinjuma alibainisha kuwa maendeleo ya mradi yanakwenda vizuri na kwamba wakandarasi wanafanya kazi kwa kasi ili kufikia malengo yaliyowekwa.

“Nimefurahi namna mradi huu unavyokwenda kwa wakati, na tunatarajia kuwa utakuwa mfano wa kuigwa kwa miradi mingine,” aliongeza.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mwinjuma aliambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, ambapo alijibu baadhi ya maombi ya mbunge huyo, akiwataka wakandarasi kuhakikisha kuwa watu wanaozunguka mradi huo wanapata manufaa.

“Hakikisheni pia kuwa wananchi wa maeneo haya wanapata faida zaidi kutokana na mradi, ikiwa ni pamoja na ajira za kimkataba, maana wao ndio wenyeji wa mradi huu.
"Aidha, niwaombe muwasaidie wakinamama wanaofanya biashara ya chakula katika eneo hili kwa kuweka mabomba ya maji nje ya uwanja ili wasiangaike kuingia ndani kwa ajili ya maji, badala yake wayachukue kwa urahisi wakiwa nje,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news