NA LUSUNGU HELELA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa kanzidata za wanafunzi waliohitimu Vyuo Vikuu waliotoka kaya za walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100 katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Amesema, lengo la Serikali la kuandaa kanzidata hiyo ni kutaka kuwa na takwimu sahihi na kuendelea kufuatilia maendeleo yao ya kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.
Mhe. Sangu ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi pamoja na walengwa wa TASAF baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia Mradi wa TASAF katika Kata ya Iziwa na Kata ya Tembele zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Amesema, hatua hiyo inakuja kufuatia TASAF na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na kuweza kuunganisha kanzidata zake ili kuwezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za walengwa kutambulika kirahisi na kuwa wanufaika wa Mikopo hiyo ya elimu ya juu kwa asilimia 100.
Mhe. Sangu amesema kwa mujibu wa takwimu jumla ya wanafunzi 11,524 kutoka Kaya maskini zilizotambuliwa na TASAF wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100.
“Idadi hiyo ya wanafunzi waliopata mkopo huo ni kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2024/2025, kitendo ambacho kimepelekea watoto hao kutimiza ndoto zao za kujiendeleza kielimu ikizingatiwa kuwa ni wa kutoka katika kaya maskini’’.
Amesema,Serikali kupitia HESLB imeweza kutambua na kuendeleza rasilimali watu kutoka Kaya maskini katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo jukumu la Mamlaka za Serikali za Mitaa kujua maendeleo yao pindi wanapohitimu.
Ameongeza kuwa idadi hiyo ya wanafunzi waliopata mikopo kupitia TASAF ni mafanikio makubwa yaliyopatikana, ikiwa ni siku chache zilizopita tangu HESLB ilipoadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika mkutano huo,mmoja wa wahitimu kutoka Chuo Kikuu cha Mbeya (MUC),Obeid Mwasaga amesema alianza kunuafaika na TASAF akiwa darasa la kwanza lakini baada ya kudahiliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakuwa na taarifa kuwa kupitia TASAF anaweza kupata mkopo, hivyo alilazimika kuacha chuo akiwa mwaka wa pili kwa kushindwa kulipa ada na baadae alijiunga na MUC baada ya kuandikiwa barua na TASAF.
