NEMC mbioni kuwa mamlaka

DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu Wa Rais -Muungano na Mazingira Hamad Masauni amesema serikali imeyapokea na inaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo matatu ya marekebisho ya Sheria ya Mazingira sura 191.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kanuni ya kulifanya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa Mamlaka, umuhimu wa kutunga Sheria ya Uchumi wa Buluu na kutambuliwa kisheria kwa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).

Masauni amesema hayo wakati akichangia taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kwa Mwaka 2024 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Jackson Kiswaga bungeni jijini Dodoma.

Pia Masauni ameipongeza Kamati hiyo kwa mchango wake na kusema kuwa ni wenye maono katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya uhifadhi wa mazingira.

Amesisitiza kuwa dhamira ya serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na Kamati hiyo.

“Kama ambavyo tuliwaahidi kwenye kamati, Mheshimiwa Spika naomba mbele yako niahidi tutayafanyia kazi yale yote mliyotushauri wakati wa michango ya wabunge na taarifa ya kamati,

"Tayari tumeandaa mpango kazi kabambe ambao mpaka leo tunavyozungumza hakuna hata kipengele kimoja hatujakitekeleza kama tulivyojipangia kwa hiyo tunakwenda vizuri,” amesema.

Masauni amesema kuwa ni matamanio ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuona maeneo hayo matatu yaliyoainishwa ikiwezekana Bunge lijalo kwa ushirikiano mkubwa lipitishe.

Awali, akiwasilisha taarifa hiyo Kiswaga amesema azimio la Bunge kuwa Serikali itoe mafunzo kwa wataalamu wa ndani wawe na ujuzi wa kuandaa mapitio ya tathmini ya athari kwa mazingira limetekelezwa kikamilifu.

Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga amesema Ofisi ya Makamu wa Rais katika kipindi cha Februari hadi Desemba 2024 imetoa mafunzo hayo kwa jumla watumishi 75.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news