DODOMA-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeshiriki katika Mkutano maalumu wa Majadiliano ya Kimkakati ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050. Mkutano huo umefanyika tarehe 28 Februari, 2025 jijini Dodoma.
Mkutano huo uliwahusisha Mawaziri kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini.


Akizungumza mara baada ya Mkutano huo, Mwandishi Mkuu wa Sheria,Bw. Onorius J. Njole ambaye alimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kikao hicho, amesema kuwa katika mkutano huo wameweza kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kuimarisha uhusiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Washirika wa Maendeleo.
“Tumeweza kujadili na kuona ni namna gani kama nchi inaweza kuendelea kunufaika na misaada mbalimbali au na mashirikiano baina ya Serikali na Washirika na Maendeleo,"amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Aidha, Mwandishi Mkuu wa Sheria ameeleza kuwa majadiliano hayo pia yameangazia namna nchi inaenda kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 ambayo iko kwenye maandalizi, ambapo utekelezaji wa Dira hiyo unategemea misingi na mifumo ya kisheria hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina nafasi kubwa katika kuifikia Dira ya Taifa ya 2050.
"Utekelezaji wa Vision 2050 kwa kiasi kikubwa unategemea mifumo mbalimbali ya kisheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatarajia kuwa kiungo kikubwa katika utekelezaji wa jambo hilo,”ameeleza Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Sambamba na hilo, Bw. Njole amesema kuwa mkutano vilevile umejadili na kuyaangalia maeneo ya Siasa, Demokrasia na kukuza uwekezaji ambapo masuala hayo yataanza kutekelezwa na Washirika wa Maendeleo.