DODOMA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa katika sekta ya michezo, habari, utamaduni na sanaa.

Aidha, amepongeza jitihada za Rais Samia katika kuboresha miundombinu ya michezo kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo. Ameeleza kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni 92.7 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha, ambao umefikia asilimia 25 kukamilika. Kufikia Desemba 2025, majukwaa yote yatakuwa tayari, na ifikapo Juni 2026, uwanja utakuwa umekamilika kikamilifu.
Kwa upande wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Prof. Kabudi ameeleza kuwa ukarabati wake umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi ametangaza kuwa Februari 13, 2025, Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa Uwanja mpya wa Dodoma katika eneo la Nzuguni. Mkandarasi tayari amepatikana, na Rais Samia ameshatoa fedha za kuanza mradi huo. Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 32,000 kwa wakati mmoja.
Mbali na uwanja huo, eneo hilo litakuwa na kituo cha michezo changamani kinachohusisha aina mbalimbali za michezo, ambacho ujenzi wake tayari umefikia asilimia 67.
Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha sekta ya michezo ili kukuza vipaji na kuiweka Tanzania katika ramani ya michezo kimataifa.