ADDIS ABABA-Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Kenya,Mheshimiwa Raila Odinga amekubali matokeo ya uchaguzi wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambapo alishindwa na Mahamoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti.
Ni kupitia uchaguzi uliofanyika usiku wa Februari 15,2025 jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Katika raundi ya kwanza ya uchaguzi, Raila Odinga alipata kura 20, Mahamoud Ali Youssouf alipata kura 18, na Richard Randriamandrato wa Madagascar alipata kura 10.
Nchi moja ilikosa kupiga kura. Katika raundi ya pili, Raila alipata kura 22, Youssouf alipata 19, huku Randriamandrato akipata kura saba.
Aidha,katika raundi ya tatu, Youssouf alichukua uongozi kwa kura 23, Raila akipata 20, na Randriamandrato akipata kura 5, huku nchi moja ikikosa kupiga kura.
Katika raundi ya nne, Youssouf alipata kura 25, Raila alipata kura 21, na kura moja ikaharibika. Waliokosa kupiga kura walikuwa mataifa mawili.
Pia,katika raundi ya tano, Youssouf alipata kura 26, Raila alipata 21. Hakukuwa na kura zilizoharibika, lakini taifa moja lilikosa kupiga kura. Katika raundi ya sita, Youssouf alipata kura 26, Kenya ilipata kura 22, huku taifa moja likikosa kupiga kura.
Vilevile,katika raundi ya saba, Mahamoud Ali Youssouf alipata kura 33 na alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya AUC.
Mheshimiwa Raila Odinga alisema anakubali matokeo hayo huku akisisitiza kuwa, hiyo ni ishara ya kuimarisha demokrasia barani Afrika
Wakati huo huo, Raila Odinga amebainisha kuwa, yupo tayari kushauri au kutoa usaidizi wa kitaalamu kadri atakavyohitajika katika kamisheni hiyo.
Mshindi
Mahamoud Ali Youssouf alishinda uchaguzi huo baada ya kupata kura 33 katika raundi ya saba akimshinda Raila Odinga ambaye alijiondoa katika raundi ya sita.
Youssouf alikubali ushindi wake na alisema kwamba anajivunia kushinda uchaguzi huo na anatarajia kufanya kazi kwa bidii katika kuendeleza demokrasia na ushirikiano wa Bara la Afrika.