ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Benki ya Dunia kwa msaada wa kiasi cha dola milioni 100 kwa ajili kuimarisha miundombinu ya Sekta ya Afya hapa nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Mkurugenzi Muendeshaji wa Benki hiyo Kanda ya Kusini Mwa Afrika, Milena Stefanova na ujumbe wake Ikulu Zanzibar leo Februari 18,2025.

Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameuelezea Ujumbe huo kuwa Serikali ina Malengo Mahsusi ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo Bora cha Matibabu kwa Nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa Ujumla na kuipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande mwingine Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazroui ameeleza kuwa Wizara hiyo inajipanga vema kuhakikisha fedha hizo zinaenda kutumika kufanikisha lengo la kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha pekee cha Utalii waTiba na Matibabu na Mafunzo ya Afya ( HEALING ISLAND) kama zilivyo nchi za India na Thailand.