ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili kuongeza idadi ya wawekezaji kwa kuimarisha huduma ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege, barabara,miundombinu ya maji,umeme na afya.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Hoteli ya Sandies Nungwi Beach Resort ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameziagiza taasisi, wadau na wananchi kuendelea kushajihisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili Zanzibar inufaike zaidi na mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amezitaja faida kuu za uwekezaji hapa nchini kuwa ni ukuaji wa Uchumi, Ongezeko la Watalii ,Ongezeko la Kodi na upatikanaji wa fursa za ajira hususan kwa vijana.
Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Mamlaka ya Uwekezaji ya Zanzibar (ZIPA) kwa kupunguza muda wa upatikanaji wa vibali vya uwekezaji.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ametoa rai kwa wawekezaji wote kuhakikisha miradi yao inawanufaisha wananchi kwa kuondoa matatizo yaliomo ndani ya jamii ikwemo ukosefu wa huduma za Maji Afya,Umeme na Elimu.
Hoteli ya Sandies Nungwi Beach Resort inayomilikiwa na Kampuni ya Away Hotels Zanzibar Limited kwa asilimia 99 na Paolo Ross raia wa Italia ambapo itagharimu Dola Milioni 17 hadi kukamilika Kwake ina vyumba 126 na kutoa fursa za Ajira 200.