ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.Hussein Mwinyi ametoa wito kufanyika upembuzi yakinifu wa programu za mafunzo ya amali ili kuandaa wahitimu kwa soko la ajira na mahitaji ya viwanda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemedi Ali Suleiman ameyasema hayo wakati akiwahutubia wadau wa elimu akimuakliisha Mhe. Dkt.Mwinyi katika mkutano wa Utafiti wa Elimu uliofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Maruhubi.
Alizitaja rai hizo ni pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za Elimu na Sekta Binafsi, ambapo kwa mkakati huo watapatikana wahitimu wenye ujuzi unaotakiwa sokoni.
Nyingine ni kutambua changamoto zinazowakumba vijana, hasa wanawake na makundi maalum katika upatikanaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na kuzipatia suluhisho.
Aliongeza kuwa, kuimarishwa mitaala ya elimu na mafunzo ya amali ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi na kufanya utafiti wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na teknolojia bunifu.
‘’Ni matumaini yangu kuwa tafiti katika maeneo hayo zitaiwezesha Serikali na wadau wa elimu kufanya maamuzi sahihi ya kukuza sekta ya mafunzo ya amali yatakayowapatia vijana wa Tanzania ujuzi wa kisasa wa kuchangia maendeleo ya Taifa,"alisema Dkt.Mwinyi.
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar, Prof. Moh’d Makame Haji alisema, SUZA inaongoza kwa kufanya tafiti zinazohusiana na mazingira, afya, elimu na uchumi ambazo zimeleta mchango mkubwa katika kuimarisha sera za elimu na maendeleo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, makongamano kama hili yanatoa fursa kwa watafiti, wasomi, na watunga sera kubadilishana maarifa na kuimarisha mwelekeo wa utafiti wa elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya maandalizi katika mkutano huo, Hannah Simon alisema, Utafiti Elimu Tanzania 2025 ni matokeo ya kazi kubwa ya Kamati ya Maandalizi, inayoongozwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia CoICT (UDSM-CICT), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) – kwa kushirikiana na FCDO, Canada, British Council, EdTech Hub, na Aga Khan Foundation.
Aidha, katika kongamano hilo mada kuu zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na Wanafunzi wanaoacha skuli, wanaobaki na wanaorejea skuli, Maandalizi ya Walimu, Hali ya Hewa, Mazingira na Elimu na Elimu ya Ufundi Stadi (TVET) na Uwezo wa kupata ajira.
Mkutano huo ni wa nne ambapo kwa mara ya kwanza umefanyika Zanzibar, umewashirikisha wadau mbali mbali wa elimu kutoka ndani na nje ya Tanzania umedhaminiwa na mashirika ya kimataifa na kijamii lakini pia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.