ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameisisitiza UVCCM kuendeleza kasi ya uhamasishaji uandikishaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura na kuhakikisha vijana wengi wanajiandikisha litakapoanza kwa upande wa Unguja hivi karibuni.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la Bweni la Vijana wa Kiume wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Aidha, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa ni lazima Chama nacho kiache alama ya uongozi itakayokumbukwa kwa muda mrefu kwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo na miradi ya Chama katika ngazi zote.
Halikadhalika Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa alama iliyoachwa na Serikali katika Sekta zote za Maendeleo ni lazima pia iachwe ndani ya CCM.
Vilevile Dkt.Mwinyi ameipongeza UVCCM kwa kufanikiwa kujenga Jengo hilo litakalotumika kwa harakati mbalimbali za Jumuiya hiyo.
Kwa upande mwingine Dkt.Mwinyi amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuunga Mkono juhudi za Jumuiya hiyo kwa hali na Mali ili dhamira ya kuwajenga vijana kuwa wazalendo na kuwapatia mafunzo mbalimbali ifanikiwe.