Rais Dkt.Mwinyi azindua hati fungani ya Zanzibar SUKUK, ataka wanaodai PBZ inauzwa wapuuzwe

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Serikali imeamua kwa makusudi kuwa na utaratibu wa hati fungani kuwa njia rasmi ya kuyafikia maendeleo endelevu hivyo SUKUK (hati fungani inayofuata misingi ya sharia) itaenda kufanikisha azma hiyo.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Februari 22,2025 alipozindua hati fungani ya Zanzibar SUKUK katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi katika muda mfupi ujao, hivyo kuwepo kwa Zanzibar SUKUK kutaipa Serikali uwezo na uhakika wa kupata fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.
Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa, nchi nyingi zilizoendelea duniani zimefanikiwa kwa kupitia mfumo huo wa SUKUK unaozingatia misingi ya Sharia.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, lengo ni kuimarisha uwezo wa Zanzibar kiuchumi na kuwasisitiza wananchi, wadau na taasisi za umma na binafsi kuchangamkia fursa hiyo inayompa mdau faida ya asilimia 10.5 kila mwaka kuwa njia muhimu ya kujiimarisha kiuchumi.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,mafanikio ya hatua hiyo yanahitaji ushiriki wa wananchi wengi watakaonunua Hatifungani za Zanzibar SUKUK na kuwahakikishia kuwa ipo katika hali nzuri.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kukanusha taarifa potofu zinazosambazwa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuwa, Serikali inakusudia kuiuza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Ameeleza kuwa, kinachofanyika ni kuijengea uwezo benki hiyo ili iwe na mtaji mkubwa zaidi wa kuikopesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news