ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amesema, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, kitakachofanyika siku ya Machi 6,2024 katika viwanja vya Maonesho vya Dimani-Nyamanzi ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Ameyasema hayo leo Februari 27, 2025 katika Ukumbi wa Wizara uliopo Kinazini jijini Zanzibar wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
"Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni kipenzi cha Wazanzibari, Mheshimiwa Dkt,Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi."
Waziri Pembe amesema kuwa, kwa mwaka huu wa 2025 kwa upande wa Zanzibar Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto itaadhimisha siku hiyo katika viwanja hivyo vya maonesho ambapo shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika kuelekea katika maadhimisho hayo.
Amesema, miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali, maonesho ya wajasiriamali ambayo yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Kisonge.
Vilevile,kutoa vipindi mbalimbali vya redio na tv, pia uzinduzi wa Muongozo wa Uanzishwaji wa Majukwaa pamoja na Uzinduzi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambayo yameundwa hivi karibuni nchi nzima.
"Majukwaa haya yameanzishwa yakiwa na lengo lilelile la kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na mafunzo ya kuhamasisha masuala ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia."
"Aidha, uzinduzi wa muongozo wa uundaji na uendeshaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi unakwenda sambamba na siku hii muhimu ya wanawake duniani."
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi, ambapo dunia nzima huadhimisha siku hii kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa maazimio ya Kimaifa, Kikanda na Kitaifa.
"Kwa upande wa Tanzania nzima kilele cha maadhimisho haya ya siku ya mwanamke kitafanyika siku ya tarehe 8 Machi katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid Arusha na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Maadhimisho haya ni fursa adhimu ya wanawake kutoka mikoa mbalimbali kuungana, kubadilishana uzoefu, na kujadili mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili, hususan katika nyanja za kiuchumi."
Ameongeza kuwa, maadhimisho haya pia huwa na lengo la kuendelea kutathmini juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi na kupanga mikakati mipya ya kupambana na kadhia hii.
"Kwa kawaida maadhimisho haya kwa kila mwaka huwa na ujumbe au kaulimbiu maalum unaoakisi mikakati ya kuondoa tatizo hilo."
Amesema, kauli mbiu ya mwaka huu wa 2025 inasema Ushiriki wa Mwanamke na Msichana ni kichocheo cha Maendeleo.
"Ujumbe huu unatupa fursa ya kuchochea na kushajihisha wanawake kujitokeza kushiriki katika shughuli za Uchumi, Kijamii na Kisiasa ambavyo vyote kwa ujumla vinalenga kuchochea maendeleo."
Waziri Pembe amesema, pia ujumbe huu unasisitiza haja ya kuwekeza kwenye masuala ya kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali vya wajasiriamali sabambamba na kuangalia masuala ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
"Nipende kuwaomba wananchi wote wa Zanzibar hasa wanawake mkiwemo nanyi ndugu zangu waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi kujumuika nasi katika Maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
"Taifa imara linalojitegemea kiuchumi hupelekea kuwa na wananchi imara wakiwemo na wanawake imara wanaojitegemea kiuchumi. Na sisi Zanzibar tunajivunia Rais wetu ambaye anasimamia kuona wananchi wake wamesimama imara tukiwemo nasi wanawake."