NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka historia nyingine katika Sekta ya Maji baada ya kutekeleza mradi wa maji wa Bwawa la Kidunda ambao ulishindikana zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Mradi wa Bwawa la Kidunda uliasisiwa tangu enzi za Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mwalimu Julius Nyerere kuanzia mwaka 1961.
Utafiti wa kwanza wa ujenzi wa mradi huo uliopo Morogoro Kusini ulifanyika mwaka 1961 na Shirika la Chakula Duniani (FAO) ukihusisha maji ya Bonde la Mto Ruvu.
Utafiti wa pili ulifanyika mwaka 1962, na ulifanywa na wataalamu kutoka nchini Ufaransa ambao walifanya mapitio ya taarifa ya awali na wakachagua maeneo ya Mkombezi, Mgeta, Ngerengere na Kidunda ya utekelezaji wa mradi.
Utafiti wa tatu ulifanywa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na walibainisha maeneo hayo hayo sawa na utafiti wa pili.
Licha ya jitihada hizi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, mradi huu haukufanikiwa kutekelezwa, na hata katika awamu zilizofuata mradi pia haukuweza kutekelezwa kutokana na sababu mbalimbali.
Historia ya mradi huu imekuja kuwa dhahiri katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikiwa kuruhusu utekelezaji wa mradi huu kwa kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 336 zitumike kutekeleza mradi huu.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA),Mhandisi Mkama Bwire katika ziara ya wahariri na wanahabari iliyoangazia kuangalia utekelezaji wa mradi huo wa Bwawa la Kidunda ameendelea kumshukuru Rais wa Dkt.Samia kwa kuonesha upendo kwa wananchi wake.
"Na hili kwa kweli tuna haki ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa sababu bwawa hili lilikuwa kwenye makaratasi tu tangu tumepata Uhuru mwaka 1961,lakini limekuja kutekelezwa katika hii Awamu ya Sita."
Mhandisi Bwire amesema, bwawa hilo ujenzi unaendelea ambapo kwa sasa wapo zaidi ya asilimia 27 za utekelezaji.
"Bwawa hili, kama mnavyofahamu katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kumekuwa na changamoto wakati mwingine wa kiangazi ya upatikanaji wa maji.
"Bwawa hili, liko katika Mkondo wa Mto Ruvu ambao ndiyo chanzo kikubwa cha maji katika maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani ambao ni zaidi ya asilimia 87 ya maji yote yanayozalishwa katika eneo hilo.
"Kwa hiyo, kutokana na changamoto ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika miaka ya nyuma ya kupungua kwa kina kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hali ya maji katika Mto Ruvu imekuwa ikileta changamoto kubwa katika uzalishaji wa maji na kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji katika shughuli za binadamu pamoja na uchumi katika maeneo hayo."
Mhandisi Bwire amesema, katika kutatua changamoto hiyo ya kuhakikisha muda wote kunakuwa na maji ya kutosha katika Mto Ruvu na hivyo kutosheleza katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, Serikali ikaamua kujenga bwawa hilo lenye uwezo wa kutunza maji lita bilioni 160 au mita za ujazo milioni 160.
Amesema, bwawa hilo pamoja na manufaa makubwa lenyewe kazi yake ni kusaidia kuzuia mafuriko ambayo yamekuwa yakijitokeza.
Pili, amesema litakuwa linasaidia kuwa na maji ya kutosha katika mitambo yao ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
"Hivyo, kuhakikisha Mkoa wa Dar es Salaam unapata maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, lakini vilevile ya viwandani."
Jambo la tatu, Mhandisi Bwire amesema ni kuhusu uwezeshaji wa shughuli za umwagiliaji ambapo eneo la karibu kuna uwekezaji mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji unaendelea.
Pia, mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 20 za umeme ambao utaingizwa katika Gridi ya Taifa.
"Hivyo, kuongeza uwezo wa umeme katika nchi yetu ili kuwa na uhakika zaidi wa nishati ya umeme."
Vilevile, mradi huo umewawezesha utekelezaji wa mradi wa barabara zaidi ya kilomita 75 kwa kiwango cha changarawe kutoka Ngerengere hadi Kidunda.
"Ujenzi wa barabara hii nao unasaidia kuinua hali ya uchumi ya watu ambao wapo kando kando ya barabara, kama mnavyoona huku vijijini shughuli za kilimo zinaendelea hivyo watu wataweza kuzalisha mazao yao na kuweza kuyafikisha kwenye masoko."
Pia, amesema uwepo wa bwawa hilo utasaidia kwa jamii ambayo ipo kwenye maeneo hayo kuweza kufanya shughuli za uvuvi kulingana na taratibu zitakazowekwa na Wizara ya Uvuvi.
"Lakini, nako itajaribu kulinda mazingira ya huku hivyo kuwezesha shughuli za kitalii."
Shughuli ambazo, Mhandisi Bwire amesema kuwa, zitasaidia kukuza uchumi wa nchi.
"Kwa hiyo, hayo ni baadhi tu ya manufaa tunayoyaona ya moja kwa moja ukiachana faida zingine za watu watakaohusika katika shughuli za ujenzi na ajira.
"Kwa kipekee tunashukuru sana kwa Serikali, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa maamuzi hayo, lakini tunaishukuru Wizara ya Maji chini ya Mheshimiwa Aweso ambaye ni waziri wetu kwa miongozo ambayo amekuwa akitupa kuhakikisha suala hili linakwenda.
"Na sasa hivi tunaendelea vizuri na tunatarajia kwa jinsi tunavyoendelea ikifika Juni 2026 basi ukamilishaji wa bwawa hili uweze kukamilika na matokeo hayo tuweze kuyaona."
Balile
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatius Balile amesema kuwa, kukamilika kwa bwawa hilo kutaleta suluhisho la upatikanaji wa maji ya uhakika jijini Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa na mamlaka hiyo.
"Tulikutana na Mtendaji Mkuu wa DAWASA kama mwezi mmoja na nusu hivi pale Dar es Salaam, kwa muda mrefu sana vyombo vya habari vilikuwa vikiandika juu ya ukame, mgawo wa maji, upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
"Lakini, mara kwa mara vilikuwa vikirejea kwamba suluhisho la tatizo hili la maji katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa jirani ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda.
"Na kama alivyosema Afisa Mtendaji Mkuu kwamba hili bwawa lilifanyiwa utafiti wa kwanza mwaka 1961, halikupata kujengwa, liliendelea kuwapo likawa kwenye vitabu na maandishi, lakini Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya vyombo vya habari kuendelea kuandika."
Balile amesema, maji ambayo yanatoka kwenye visima hayawezi kutosheleza uhitaji ndiyo maana Serikali ikasikia na ikaamua kujenga mradi huo.
"Ni mradi ambao ni ukombozi wa muda mrefu kwa Jiji la Dar Es Salaam, kwa maana ya kwamba pale mradi utakapokuwa umekamilika Juni, mwakani inamaana suala la mgawo wa maji Dar es Salaam hadi hapo idadi ya watu itakapokuwa imeongezeka itakuwa ni historia.
"Kwamba Mto Ruvu ambao unatoa asilimia 87 ya maji utakuwa hauwezi kupungukiwa maji, maji yatakuwepo muda wote.
"Kwa hiyo, wakati tunaipongeza Serikali ya Rais Samia, vyombo vya habari tuvishukuru pia kwa kuendelea kufanya kazi hii bila kuchoka kwa kuendelea kueleza kwamba wananchi wa maeneo mbalimbali hawana maji...
"Maji yamekauka katika Mto Ruvu na hii imefikisha Serikali mahali ikasikia kwamba kuna kilio huko kwenye jamii, watu wanahitaji Bwawa la Kidunda lijengwe.
"Miradi kama hii mikubwa ambayo inahitaji fedha nyingi na utaalam tunaamini kwamba itaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali na hapo Serikali itakuwa imetimiza vema wajibu wake wa kuwahudumia wananchi ambao ni kuhakikisha kwamba wanapata huduma za jamii ikiwemo maji,"amesema Balile.
Bonde la Wami
Naye Janeth Kisoma ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu amesema,wao jukumu lao kubwa ni kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Majukumu hayo wanayatekeleza chini ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009 na marekebisho yake Na.8 ya mwaka 2022.
Amesema, Bwawa la Kidunda ni miongoni mwa vyanzo vya maji ambavyo ni 283 ambavyo vinasimamiwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu.
Vyanzo vingine vya maji amesema ni pamoja na mabwawa, mito, chemichemi na maeneo mengine.
"Kwa maana hata maji yaliyoko chini ya ardhi kama vile visima, pia vyote vinasimamiwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu.
"Lazima tusimamie ugawaji wa rasilimali za maji kwa kuwa watumiaji wa maji ni wengi ili kila mtumiaji aweze kupata kiasi cha maji kutokana na kiasi kingine cha maji ambacho kinatakiwa kibaki katika mito yetu kwa ajili ya matumizi mengine.

"Hivyo, sisi kama Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu kwa suala la Bwawa la Kidunda tupo tayari na tumejipanga kikamilifu kuupokea mradi huu ili kuhakikisha tunausimamia vizuri ili kuhakikisha kiasi cha maji kitakachokuwepo katika Bwawa hili hakitapungua.
"Bwawa hili litapata maji ya kutosha,katika misimu yote na Bwawa hili litakuja kuwa mkombozi hasa kipindi cha kiangazi."