DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuongeza imani na amani kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kwa Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program) sambamba na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka wahitimu hao kuwa chachu ya maendeleo katika jamii na kutumia elimu na stadi za uongozi walizopata kunufaisha jamii kwa ujumla.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amewarai wanawake kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali na kuwataka kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwa waaminifu katika kulipa kodi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya mwananchi.

Matukio mbalimbali kwenye Maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanza kwa mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program) pamoja na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam tarehe 21 Februari, 2025.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Samia amewahamasisha wanawake wenye sifa na uwezo kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.