SIMIYU-Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni tiba ya maendeleo hivyo watanzania wanapaswa kwenda nae kwani ataifikisha nchi kule kunakotarajiwa.

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayeona, kusikiliza na kutatua changamoto za Watanzania kwa ustadi wa hali ya juu na amedhihirisha hilo katika kipindi chake cha uongozi.
Ametoa kauli hiyo leo Februari 16, 2025 wakati Mkutano Mkuu Maalum Chama cha Mapinduzi Jimbo la Maswa Mashariki, uliofanyika katika uwanja wa nguzo nane,Maswa mkoani Simiyu.

Akizungumzia Sekta ya Maji Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imedhamiria kuhakikisha inatekeleza miradi mikubwa ya maji kutoka katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa maji safi na Salama.
“Mpango wetu ni kuendelea kufikisha huduma ya maji mpaka vitongojini.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika sekta ya afya Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa na kuwapunguzia adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa Umeme inaimarika nchini, Serikali imeendelea kutekeleza miradi umeme.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa chama hicho kipo imara na kinaendelea kuwahudumia Watanzania.
Amesema kuwa kutokana na sera imara zinazotekelezaka za chama hicho, kimeendelea kufikisha huduma na mahitaji muhimu kwa Watanzania.
