Rais Kagame na Tshisekedi kukutanishwa Dar mgogoro wa DRC

NAIROBI-Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Ni kwa ajili ya mkutano wa kujadili mgogoro unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Rais Ruto amesema,marais waliokubali kuhudhuria mkutano huo ni; Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, Paul Kagame wa Rwanda.

Pia,yumo Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda na Hassan Mohamud wa Somalia.

Rais Ruto amesema, lengo lingine ni kujadili amani na usalama katika nchi za ukanda wa jumuiya hizo mbili.

Mbali na hayo, kwa mujibu wa BBC baada ya miezi kadhaa ya mapigano, waasi wa M23 sasa wanaudhibiti mji mkuu wa Goma, mji unaokaliwa na zaidi ya watu milioni mbili, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakati M23 walipowasili mjini Goma, hawakupata upinzani mkali kutoka kwa jeshi la serikali ya DRC. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 700 wameuawa tangu M23 kuingia Goma.

Aidha,mamia ya wengine nao walijeruhiwa huku maelfu wakikimbilia maeneo mengine ya nchi jirani.

Mji huu ambao huwa na shughuli nyingi sasa umesalia mahame. Maduka mengi yamefungwa, shule, benki, ofisi za serikali na zile za mashirika yasiyo ya kiserikali zimefungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news