RAS Musabila akagua miradi ya maendeleo Butiama

MARA-Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kukagua ujenzi unaoendelea katika Shule ya Sekondari ya Butuguri na Shule ya Amali ya Mkoa wa Mara.
Katika Shule ya Sekondari ya Butuguri, Bwana Kusaya amekagua ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo kwa ajili ya mapaokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2025 na kupongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuongeza kasi ya ujenzi.

Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mgango- Kiabakari kuhakikisha shule hiyo inapata maji ya uhakika kabla ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.

Katika Shule ya Amali ya Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Mkoa amekagua mradi huo unaendelea kujengwa katika Kijiji cha Butiama na kupongeza kwa kazi inayoendelea na kumtaka Mkurugenzi wa Wilaya ya Butiama kuongeza kasi ya ujenzi ili shule hiyo ianze kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari, 2026.
Aidha, Bwana Kusaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama kufanya utaratibu wa kuongeza eneo zaidi kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo ili kuweza kukidhi mahitaji halisi ya Shule za Amali za Mkoa.

“Hili eneo la ekari 40 ninaliona ni dogo, shule za amali zinakuwa na majengo mengi zaidi ikiwemo nyumba za walimu, hili eneo halitatosha, fanyeni utaratibu mliongeze” amesema Bwana Kusaya.

Bwana Kusaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kukamilisha miradi hiyo ndani ya miezi miwili na atarudi tena kukagua miradi hiyo tarehe 17 Aprili, 2025 ili kuona maendeleo yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Butuguri Mwal. Nyamtelele Christopher amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 shule hiyo imepokea jumla ya shilingi 510,448,303.78 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu, vyumba vya madarasa saba, matundu nane ya vyoo na fedha za ukamilishaji wa darasa moja.

Mwal. Christopher amesema fedha hizo zimetoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo EP4R II, Serikali Kuu na SEQUIP na zilipokelewa kwa awamu tofauti tofauti na mpaka sasa bweni moja na vyumba vinne vya madarasa vimekamilika, huku mabweni mawili yapo kwenye hatua za msingi.
Mwal. Christopher amesema ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa vinne vipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na wanategemea kukamilisha mradi huo ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.

Mwal. Christopher amesema shule hiyo kwa sasa inachangamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya ujenzi na matumizi ya wanafunzi wa kutwa wanaosoma hapo na kuwa wanatumia gharama kubwa kununua maji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Butiama Mwal. Grace Isomba ambaye pia ni msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Amali Mkoa wa Mara amesema mradi huo ulipokea fedha shilingi bilioni 1.6 mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mwal. Isomba amesema fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu 13 ikiwemo vyumba vya madarasa (08), jengo la utawala, maabara mbili, ofisi za walimu mbili, nyumba moja ya walimu, maktaba, chumba cha Tehama, Mabweni manne, bwalo na jiko, vyoo matundu 08, karakana za ufundi tatu na tenki la maji.

Mwa. Isomba amesema mpaka sasa mradi huo umetumia shilingi 353,491,943,04 na kubakiwa na shilingi 1,246,508,056.96 kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huo.

Katika ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa aliambatana Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Butiama, Mkurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news