RC Makongoro Nyerere amlilia Sam Nujoma

RUKWA-Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameungana na viongozi wengine barani Afrika kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Namibia hayati Samuel Shafiishuna Daniel Nujoma.Mheshimiwa Makongoro amuelezea hayati Nujoma kama kiongozi shupavu aliyechangia kwa kiasi kikubwa ukombozi wa Bara la Afrika.

Kupitia ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Mheshimiwa Makongoro ameandika;

"....nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mzee Sam Nujoma, Rais wa Kwanza wa Namibia na shujaa wa ukombozi wa Bara letu la Afrika.

Mzee Nujoma hakuwa tu kiongozi wa Namibia, bali alikuwa nguzo muhimu katika harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika.

Alisimama imara kupigania uhuru wa taifa lake, akiongoza SWAPO kwa ujasiri na uadilifu wa hali ya juu.

Urafiki wake na Tanzania, hususan kwa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa harakati za ukombozi, ni ushahidi wa mshikamano wa Kiafrika uliojengwa kwa misingi ya haki na usawa.

Kwa ndugu zetu wa Namibia, tunawapa pole kwa msiba huu mzito. Afrika imempoteza mmoja wa mashujaa wake wakubwa, lakini mchango wake utaendelea kuishi milele katika historia yetu.

Tuendelee kudumisha misingi ya haki, umoja na maendeleo aliyoyapigania.Pumzika kwa Amani. Mzee Sam Nujoma, kazi yako imeonekana..."

Sam Nujoma, ambaye aliongoza Namibia kutoka 1990 hadi 2005, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Alijulikana kwa juhudi zake za kuikomboa Namibia kutoka utawala wa kikoloni na aliheshimika kama mmoja wa viongozi mashuhuri wa Afrika waliopigania uhuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news